Kardinali Pengo apata mrithi wa jimbo lake

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Yuda Thaddeus Ruwa’Ichi, ameteuliwa kuwa mrithi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Uteuzi huo uliofanywa na Baba Mtakatifu Francisko, ulithibitishwa jana na Balozi wa Vatican nchini na kutangazwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Akizungumza na gazeti hili jana, katibu mkuu wa TEC, Padri Raymond Saba alisema uteuzi huo unamaanisha kuwa, Askofu Mkuu Ruwa’Ichi sasa atakuwa mrithi wa Askofu Mkuu wa Dar es Salaam atakapostaafu.

“Jimbo halitakuwa na maaskofu wawili kwa sasa, ni mpaka hapo Kardinali atakapostaafu,” alisema katibu mkuu huyo.

Kwa mujibu wa Padri Richard Mjigwa, wa Redio Vatican, Askofu Ruwa’Ichi hatasimikwa tena kama wanavyosimikwa maaskofu wengine wanaoteuliwa kwenda kuongoza majimbo, bali atachukua madaraka ya kuongoza jimbo moja kwa moja.

Gazeti hili lilipomtafuta Askofu Ruwa’Ichi kwa njia ya simu kuzungumzia uteuzi wake, alijibu kwa ufupi: “Bado natafakari kwanza.”

Hata hivyo, Oktoba 16, 2014, Mwananchi lilimnukuu Kardinali Pengo alipozungumza na waamini wa jimbo lake kuwa hawana sababu ya kuingiwa wasiwasi kuhusu hali yake ya afya kwa kuwa anastaafu miaka mitano ijayo.

Aliyasema hayo alipokuwa akihubiri katika misa iliyoandaliwa na Utume wa Wanaume Wakatoliki (Uwaka) jimboni humo.

Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 70, alisema anajiandaa kustaafu kisheria, jambo ambalo halina sababu ya kuwaweka roho juu waumini.

Kwa mujibu wa Sheria za Kanisa Katoliki, Askofu anapaswa kustaafu anapotimiza miaka 75. Kardinali Pengo alizaliwa Agosti 5, 1944. Atatimiza miaka 75 mwakani.