Katiba, Muungano vyawasubiri Makamba, Profesa Kabudi

Muktasari:

Mambo hayo hayakuibuka katika bajeti tatu zilizopita za Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Utumishi na Utawala Bora.

Dodoma. Hoja za uharibifu wa mazingira, kero za Muungano na kukwama kwa mchakato wa Katiba mpya ni mambo yanayotarajiwa kuchukua sehemu kubwa ya mjadala wa bajeti za Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Katiba na Sheria.

Mambo hayo hayakuibuka katika bajeti tatu zilizopita za Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Utumishi na Utawala Bora.

Masuala hayo yamekuwa katika mijadala na maswali ya wabunge, na hivyo kuweka uwezekano mkubwa wa kutawala bajeti za wizara hizo, zinazoongozwa na January Makamba (Ofisi ya Rais) na Profesa Palamagamba Kabudi (Sheria na Katiba). “CCM inaonekana kutokuwa na mpango na suala la Katiba mpya,” alisema Mbunge wa Malindi (CUF), Ali Salehe.

“Lakini kuna masuala ambayo licha ya kuwapo makubaliano ni muhimu yaingizwe kwenye Katiba.”

Alitoa mfano wa suala la mgawanyo wa ajira kuwa licha ya makubaliano ya kuwapo kwa mgawanyo wa nafasi 79 kwa 21 kati ya Bara na Zanzibar, suala hilo linatakiwa liingizwe kwenye Katiba.

Mbunge huyo alisema suala jingine ni la ndoa za utotoni, hasa baada ya Mahakama Kuu kuiagiza Serikali iifanyie marehebisho Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na kuongeza umri wa kuolewa kutoka miaka 14 hadi 18.

Alisema pamoja na agizo hilo, Serikali imekaa kimya na muda uliotolewa umekwisha kwa hiyo ni lazima wabunge watakuwa wakali kulizungumzia.

Mbunge huyo alisema tatizo la umri katika masuala ya ndoa limebaki kwa nchi nane barani Afrika na hivi karibuni Malawi na Bangladesh zilibadili Katiba na kuongeza umri huo.

“Hata Sadc imepitisha sheria ya kutambua umri wa mtoto kuwa ni hadi miaka 18, kwa hiyo ni suala kubwa la kujadiliwa,” alisema.

Mbunge huyo alisema katika hoja ya sheria, suala la mazombi yanayotishia maisha ya watu visiwani Zanzibar nalo litajitokeza.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Devotha Minja pia alizungumzia Katiba mpya, ambayo mchakato wake kwanza ulisusiwa na wajumbe kutoka vyama vinne na baadaye kukwama katika hatua ya kupiga kura ya maoni.

“Bila kuonyesha fedha kwa ajili ya kukamilisha Katiba mpya, kutaibuka mjadala mkubwa katika bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Wananchi wanahitaji kufahamu kuhusu ukamilishaji wa mchakato huo,” alisema Devotha.

Alisema mchakato huo umeshatumia fedha nyingi na hivyo ni lazima wabunge watahoji kuhusu mustakabali wake.

Mbunge wa Mtambile (CUF), Masoud Abdallah Salim alizungumzia uwazi katika kumaliza kero tatu za Muungano.

“Kero za Muungano si za viongozi ni za wananchi. Wahojiwe wananchi wa Bara na Zanzibar nini kero zao,” alisema.

“Miongoni mwa kero ambazo zinalalamikiwa ni Tume ya Pamoja ya Fedha na wananchi wanataka mgawanyo wa fedha baada ya Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki kuvunjwa mwaka 1967.”

Salim alisema mgawanyo wa fedha hizo haujawekwa wazi tangu kuvunjwa kwa bodi hiyo, jambo ambalo linawafanya wananchi wahoji.

Hoja ya Katiba mpya ilizungumziwa pia na Riziki Ng’wali (viti maalumu-CUF) na ambaye pia ni katibu wa wabunge wa CUF. Alisema mkazo utabaki katika mchakato huo ambao wananchi walishashauri mfumo wa Muungano wautakao.

“Hatuwezi kuondoa kero za Muungano kwa vikao, kwanza vikao vyenyewe ni kero kwa sababu ni gharama. Tatizo la Muungano lipo katika mfumo wake ambao bila kuubadili na kuwa uliopendekezwa na wananchi, kero haziwezi kuisha,” alisema.

Mbunge wa Vwawa (CCM), Japheth Hasunga aliangalia zaidi suala la uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

“Watu watataka kufahamu Serikali imejipangaje katika kuondokana na hali ya kutegemea mvua kwenye kilimo,” alisema.

Pia, alisema dosari ndogondogo ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na baadhi ya watu kuhusu Muungano ambazo bado hazijatatuliwa na Serikali ni miongoni mwa mambo yatakayozua mjadala katika bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Alisema wabunge watataka kufahamu utatuzi wake umefikia wapi.

Hata hivyo, alisema anafahamu kuwa Serikali imejipanga vizuri katika kujibu hoja hizo za wabunge.

Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia alisema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika bajeti hiyo ni kero za hapa na pale zinazozungumzwa na baadhi ya watu wa Zanzibar ambazo zinatakiwa kujadiliwa na kumalizika.

Nkamia pia alizungumzia mahakama

“Na kwa upande wa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria tatizo kubwa ni katika mahakama za wilaya, hasa wilaya mpya ambazo watu wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma,” alisema.

Alitoa mfano wa Wilaya ya Chemba ambayo watu wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 160 hadi Kondoa kufuata huduma za mahakama.

“Serikali iharakishe ujenzi wa mahakama za wilaya hasa katika wilaya mpya ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa karibu. Na pia mahakama za mwanzo nyingi zina hali mbaya, zinahitaji kukarabatiwa,” alisema.