Kauli ya Ndugai kutomjulia hali Lissu yaibua mjadala

Muktasari:

  • Wakati baadhi wakihusisha jambo hilo na uhusiano wa kidiplomasia, wengine wamehoji kama Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi walikwenda kumjulia hali, iweje Spika ashindwe?

 Siku moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kueleza sababu za kushindwa kwenda kumjulia hali mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyelazwa katika Hospitali ya Nairobi, Kenya, wasomi na wanasiasa wamehoji ufafanuzi wake.

Wakati baadhi wakihusisha jambo hilo na uhusiano wa kidiplomasia, wengine wamehoji kama Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi walikwenda kumjulia hali, iweje Spika ashindwe?

“Bunge si Spika pekee, yupo naibu Spika, wenyeviti wa kamati, kamati ya uongozi, wabunge na wenyeviti wa kamati,” alisema Profesa Benson Bana wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) na kuongeza “Jambo la msingi ni kumuombea Lissu apone na kurejea katika majukumu ya kibunge.”

Juzi, katika mkutano wake na wanahabari mjini Dodoma, Spika Ndugai alisema sintofahamu iliyojitokeza nchini Kenya baada ya uchaguzi mkuu ilikuwa kikwazo kwake kwenda kumjulia hali Lissu.

Alisema sintofahamu hiyo ilisababisha wanasiasa kwenda mahakamani hivyo kufanya uchaguzi mkuu kurudiwa na kuzua malumbano yaliyofanya kuwa na ‘Serikali kama ya mpito’.

Alibainisha kuwa wabunge wanaweza kwenda Kenya wanavyotaka ilimradi wawe na hati ya kusafiria lakini yeye hawezi kufanya hivyo bila kuwa na taarifa rasmi za kiserikali na kibunge, kwamba kwa kuwa uchaguzi umeshamalizika na hali ni shwari, anaweza kwenda kumuona.

Lissu anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi alikopelekwa Septemba 7 baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana akiwa ndani ya gari kwenye makazi yake eneo la Area D mjini Dodoma.

Akizungumzia kauli ya Ndugai, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema, “Spika hana sababu ya msingi. Lissu amepigwa risasi Septemba 7 na uchaguzi wa Kenya umefanyika Agosti na wapo viongozi wengi tu waliokwenda kumjulia hali, wakiwamo mawaziri wastaafu. Kenya ni nchi salama.”

Dk Mashinji alisema Spika Ndugai anapaswa kuwaeleza Watanzania sababu nyingine huku akisema ingekuwa bora hata angeeleza kuwa alipata mshtuko kwa tukio la Lissu kushambuliwa kwa risasi, hivyo kushindwa kwenda kumjulia hali.

“Lissu si mgonjwa, amevamiwa na kupigwa risasi. Kutokana na hilo ni lazima lifanyike jambo kuokoa maisha yake. Spika alipaswa kuunga mkono hatua hiyo kwa namna yoyote ile,” alisema.

Alisema kiongozi huyo mkuu wa Bunge kutoa sababu hizo hakuwezi kumsaidia, bali anachopaswa kufanya sasa ni kuchukua hatua.

“Hakwenda kumjulia hali Lissu, tayari ameshakosea. Namshauri asihangaike na jambo hili kwa kuwa tumeshamsamehe. Kuanzia sasa atazame mambo mapya, kwa maana ya kusaka suluhisho na kutoka hapa tulipo kuhusu matibabu ya mbunge wake,” alisema.

Hata hivyo, Profesa wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut), Mwesiga Baregu alipingana na Dk Mashinji na kubainisha kuwa maelezo ya Spika huenda yamebeba hoja za kidiplomasia.

“ Spika ameliweka suala hilo kiprotokali, nilichukulia labda alijaribu kwenda halafu akashauriwa asiende ama na Kenya yenyewe au Tanzania,” alisema.

“Pengine Ndugai angeulizwa mbona hajaliweka vizuri hilo. Akitoka nchini ni lazima apate kibali cha kwenda Kenya na watu wa Kenya kujua kama Spika wa Tanzania anakwenda kwao, nachukulia kama suala la kidiplomasia.

“Kama ni kinyume cha hivyo, basi ukweli unaweza kupatikana.Inaweza kuwa na ukweli ndani yake au kusiwe na ukweli wowote ingawa alivyoeleza unaweza kumuelewa kama kweli ndivyo ilivyokuwa.”

Katika ufafanuzi wake, Profesa Bana alisema, “Sidhani kama Spika kutokwenda kumuona Lissu ni jambo jema, tunatilia maanani mazingira yaliyosababisha hali ya Lissu alivyo sasa hivi. Hata ingekuwa nani ni kitu ambacho ni cha kukemea.

“Kwenda kumuona ni jambo la kiungwana. Unaweza kwenda kumuona kama wewe binafsi na unaweza kwenda kumuona kama kiongozi wake.”

Hata hivyo, alibainisha kuwa suala la kutokwenda Kenya mapema kumuona Rais huyo wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ni jambo ambalo anapaswa kuachiwa Spika mwenyewe.

“Yapo mengi, mara Bunge halimhudumii, mara hakupata stahiki na yanatoka katika familia na sehemu nyingine... hata alipokwenda Rais mstaafu na viongozi wengine kumekuwa na mengi yaliyozungumzwa. Nadhani hayo tumuachie Spika na uongozi wa Bunge,” alisema Profesa Bana.

Katika maoni yake kuhusu kauli ya Spika, mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye ni miongoni mwa watu waliosaka maridhiano baada ya kuibuka kwa mvutano wa matibabu ya mbunge huyo wa Singida Mashariki, alisema jambo la msingi ni mwakilishi huyo wa wananchi kupata matibabu anayostahili.

“Bunge litumie utaratibu wake wa kuwahudumia wabunge na kuacha mgogoro maana mbunge kutibiwa ni haki yake. Utu na ubinadamu wa Lissu uwekwe mbele kuliko mambo mengine,” alisema.

Mbatia ambaye ni mbunge wa Vunjo alisema Bunge ni kama baba na kufafanua kuwa jukumu la baba ni kuhakikisha anawahudumia watoto wake.

“Mtoto ana wajibu wa kulelewa na kutunzwa na mzazi. Suala la Lissu kupata matibabu ni haki yake ya msingi, Bunge likifanya hivyo litajijengea heshima,” alisisitiza.