Jumapili ya maombi kwa Kenya nzima

Muktasari:

Wakati tunapoelekea Oktoba 26, tukiwa watu tunaomwogopa Mungu, tunamuomba atuongoze tutimize jukumu kubwa la kikatiba, na tutaweza.

 

Nairobi, Kenya. Rais Uhuru Kenyatta amewasihi viongozi wa dini kuongoza wananchi kuiweka Kenya katika maombi kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa marudio.

Kenyatta aliyekuwa akizungumza saa chache baada ya kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Roselyn Akombe kujiuzulu akilalamikia migawanyiko ndani ya chombo hicho, amewasihi viongozi wa dini kuwaongoza Wakenya katika maombi hayo.

Huku akionekana kuzidi kusikitishwa na uamuzi wa Mahakama ya Juu uliofuta matokeo ya ushindi wake wa Agosti 8 amependekeza Jumapili kuwa Siku ya Maombi Kitaifa.

“Njia tunayopita tangu Mahakama ya Juu ilipofanya uamuzi siyo nzuri kwa nchi yetu, lakini tumshukuru Mungu kwa kutufikisha hapa,” alisema Rais Kenyatta alipozungumza na wanahabari kwenye Ikulu jijini Nairobi.

“Wakati huu tunapoelekea Oktoba 26, tukiwa watu tunaomwogopa Mungu, tunamuomba atuongoze tutimize jukumu kubwa la kikatiba, na tutaweza.”

Jaji Mkuu David Maraga Septemba Mosi aliongoza Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya urais ya uchaguzi wa Agosti 8 na akaamuru ufanyike mwingine ndani ya siku 60.

Tangu uamuzi huo ulipotolewa kumekuwa na songombingo nyingi. Kwanza mpinzani wake mkuu Raila Odinga alitangaza kujitoa akitaka uitishwe mpya katika muda wa siku 90; pili, muungano wa Nasa anaouongoza uliamua kupinga marudio kwa maandamano.

Tatu kumekuwa na mivutano ndani ya IEBC iliyosababisha mara mwenyekiti wake Wafula Chebukati kupangua safu ya watumishi na mwishowe Kamishna Akombe ametoroka nchi na kwenda New York ambako ametangazia uamuzi wake wa kujiuzulu.

Maandamano na vurugu za vijana wa Nasa juzi zilivuruga vituo vya mafunzo kwa maofisa walioteuliwa kusimamia vituo vya uchaguzi hali iliyoongeza mvutano. Polisi wameongeza ulinzi.

Rais Kenyatta, ambaye hakutoa fursa ya kuulizwa maswali alisema, “Siku hiyo (Jumapili) tutakuwa tukiomba Baraka za Mwenyezi Mungu kwa taifa letu; tutamuomba Mungu aandamane nasi, atuongoze katika kipindi hiki na hicho kinachosubiriwa. Tutawaombea viongozi wetu kwamba wapewe hekima, utu na kwamba wazingatie amani na haki.”