Kenyatta aanza kwa kukataa vielelezo

Muktasari:

  • Kupitia kwa mwanasheria wake Melissa Ng’ania, Rais Kenyatta amesema katika kikao cha awali cha usikilizwaji wa kesi kwamba kati ya vielelezo hivyo hakuna kilichopatikana kwa kuzingatia matakwa ya kisheria.
  • Mwanasheria Kimani Muhoro wa IEBC pia aliunga mkono kuondolewa kwa barua kutoka kwenye rekodi za mahakama. Alisema barua zilizotajwa zilichaguliwa kwa makusudi ili kutunga masimulizi.

Nairobi, Kenya. Rais Uhuru Kenyatta ameanza kupambana na wanaopinga ushindi wake kwa kuiomba Mahakama ya Juu kuondoa vielelezo vitano vya mawasiliano ya ndani ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) vilivyowasilishwa kama ushahidi.

Kenyatta, katika hoja zake, amedai kwamba vielelezo hivyo ambavyo vilisambaa sana kwenye vyombo vya habari, havikupatikana kwa njia halali.

Utaratibu

Kupitia kwa mwanasheria wake Melissa Ng’ania, Rais Kenyatta amesema leo katika kikao cha awali cha usikilizwaji wa kesi kwamba kati ya vielelezo hivyo hakuna kilichopatikana kwa kuzingatia matakwa ya kisheria.

Ng’ania alisema upo utaratibu wa kupata taarifa kutoka vyombo vya serikali nchini Kenya na ni lazima uzingatiwe. Mwanasheria huyo alisema ajuavyo hakuna ushahidi unaoonyesha maombi yaliwasilishwa kwenye tume.

“Haya ni mawasiliano ya ndani. Bila kuwepo maombi, inafaa kuchukulia kwamba vielelezo hivyo vilipatikana kinyume cha taratibu,” alisema.

Aliongeza kwamba kuvipokea vielelezo hivyo kutavuruga kazi za tume na kutakuwa sawa na kuingilia uhuru wa vyombo vya uchaguzi. Mwanasheria huyo aliongeza kwamba ikiwa tume ingehitaji nyaraka hizo ziwe wazi kwa umma, zingewekwa hata kwenye mtandao wake.

Pili, Rais Kenyatta, kupitia kwa mwanasheria Fred Ngatia ametaka baadhi ya nyaraka katika kesi hiyo zilizowasilishwa siku moja baada ya muda kufanya hivyo kupita ziondolewe.

Alisema nyaraka za nyongeza na rundo jingine la nyaraka zilizowasilishwa kwa kuchelewa zisipokewe mahakamani kwa ajili ya rekodi.

“Wala sihitaji kuweka mkazo kwamba kesi ilipaswa kufunguliwa ndani ya siku saba, na siku hiyo ya mwisho ilikamilika usiku wa Novemba 6,” alijenga hoja Ngatia.

Mwanasheria huyo pia ameitaka hati ya kiapo ya James Ngodi iliyowasilishwa kuunga mkono kesi iliyofunguliwa na Njonjo Mue na Khelef Khalifa iondolewe. Alisema kuibakiza kama rejea kutazua mgogoro kwa sababu si sehemu ya rekodi.

“Kwa dhati ukiwa utaondoa nyaraka zote zilizowasilishwa mahakamani baada ya muda basi futa na baadhi ya aya kwa sababu zinazungumzia nyaraka hizo zinazopingwa,” alisema.

Mwanasheria IBC

Mwanasheria Kimani Muhoro wa IEBC pia aliunga mkono kuondolewa kwa barua kutoka kwenye rekodi za mahakama. Alisema barua zilizotajwa zilichaguliwa kwa makusudi ili kutunga masimulizi.

Muhoro alisema mahakama inapaswa kuchukia tabia kama hiyo kwani vielelezo hivyo havijakamilika.

Lakini waliofungua kesi, kupitia mwanasheria Julie Soweto, walipinga maombi ya Rais Kenyatta wakidai yeye hapaswi kuomba nyaraka hizo ziondolewe kwa sababu chanzo siyo yeye.

Soweto alisema Rais Kenyatta hajaonyesha athari atakazopata ikiwa nyaraka hizo zitapokewa na mahakama. Aliongeza kwamba nyaraka hizo zinajenga uzito katika kesi ambayo inataka kuthibitisha tume haikuwa na uadilifu.

 

 

Maombi 14

Alisema nyaraka hizo tayari ziko wazi kwa umma. Mwanasheria huyo pia aliwaambia majaji ugumu walioupata kuambatanisha nyaraka hizo tofauti na madai kwamba walichelewa.

Soweto alisema wajibu wake ni kuipatia mahakama nakala za kutosha kuhusu shauri na ndivyo walivyofanya. “Haki lazima isimamiwe bila kuzingatia hitilafu za mchakato wa kiufundi. Huu ni mchakato wa kiufundi,” alisema.

Akionekana kutoridhishwa na maelezo hayo, Jaji Mkuu David Maraga alimtaka Naibu Msajili wa Mahakama Daniel ole Keiwua kutoa msimamo sahihi.

Keiwua alisema walalamikaji walifika na seti kamili na waliwasilisha nyaraka nyingine tano siku iliyofuata.

Mahakama hiyo ikiongozwa na Jaji Mkuu Maraga, Naibu wake Philomena Mwilu, na majaji Jackton Ojwang’, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u na Isaac Lenaola watasikilia maombi mengine 14 kabla ya usikilizwaji rasmi kuanza.