Kesi mmiliki Jamii Forum kusikilizwa siku mbili

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii Forum, Maxence Melo 

Muktasari:

Katika kesi hiyo mmiliki huyo anadaiwa kulizuia Jeshi la Polisi kufanya kazi yake


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga kusikiliza kwa siku mbili mfululizo, Julai 4 na 5, kesi ya kulizuia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi, inayomkabili, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii Forum, Maxence Melo na mwenzake Micke William.

Uamuzi huo umetolewa  leo Juni 17 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya uamuzi.

“Kesi hii tutaisikiliza kwa siku mbili mfululizo kwa sababu imesimama kwa muda mrefu bila kuendelea na kumbukumbu zinaonyesha tangu Desemba mwaka jana, haijaendelea, hivyo sitaki kuona visingizio wakati wa usikilizwaji wa shauri hili,” amesema Simba na kuongeza.

“Nataka upande wa mashtaka mje na mashahidi wa kutosha ili kesi hii iweze kuisha, kwa sababu ni kesi ya muda mrefu.”

Awali, Wakili wa Serikali, Kandidi Nasua alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya uamuzi, baada ya upande wa utetezi kupinga nyaraka iliyowasilishwa na upande wa mashtaka isitolewe kama kielelezo mahakamani hapo.

 

Pingamizi hilo liliwasilishwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala ambapo alidai kuwa nyaraka iliyowasilishwa na Usama Mohamed ambaye ni shahidi wa nne katika kesi hiyo, haikukidhi vigezo.

Tayari mashahidi wanne wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao katika kesi hiyo ya jinai namba 456 ya mwaka 2016.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kuzuia jeshi la Polisi kufanya uchunguzi, kinyume na Sheria Namba 22 (2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandano Namba 14 ya mwaka 2015.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Aprili Mosi, 2016 na Desemba 13, 2016 katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni.