Kibatala awasilisha kusudio la kukata rufaa kesi ya Mbowe, vigogo Chadema

Muktasari:

Kesi hiyo iliahirishwa hadi leo hakimu atakapotoa uamuzi 

Dar es Salaam. Wakili wa utetezi katika kesi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na vigogo wengine wanane wa chama hicho, Peter Kibatala amewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa, kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuamuru upande wa mashkata kufanya marekebisho ya hati ya mashtaka ya watuhumiwa hao.

Kibatala amedai kuwa wanakata rufaa kwa sababu wao waliomba mashtaka hayo yafutwe, lakini Mahakama imeamua yafanyiwe marekebisho kwenye hati ya mashtaka.

Uamuzi huo wa Mahakama ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri. Hakimu Mashauri alitoa uamuzi huo baada ya kupitia mapingamizi manane yaliyowasilishwa mahakamani hapo na Kibatala na Jeremiah Mtobesya.

Kwa pamoja, mawakili hao wa upande wa utetezi walikuwa wakiomba mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao yafutwe kwa sababu yana upungufu wa kisheria, ikiwamo shtaka moja kuwa na makosa mawili - hoja ambayo ilipingwa na upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo, Hakimu Mashauri alikubaliana na baadhi ya hoja za upande wa utetezi kuwa katika shtaka la pili, tatu, nne, tano, sita na saba yana upungufu wa kisheria na kuamuru upande wa mashtaka kufanya mabadiliko katika hati ya mashtaka.

Baada ya kutoa uamuzi huo, wakili Kibatala aliieleza Mahakama kuwa hawajaridhishwa na uamuzi huo hivyo aliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

Kibatala alidai kuwa wanakata rufaa kwa sababu wao waliomba mashtaka hayo yafutwe lakini Mahakama imeamua yafanyiwe marekebisho kwenye hati ya mashtaka.

Baada ya Kibatala kueleza hayo, wakili wa Serikali, Paul Kadushi alidai kuwa huo ni uamuzi mdogo ambao hauwezi kumaliza kesi na kwamba hawawezi kuukatia rufaa.

Kibatala alisisitiza kuwa kwa kuwa Mahakama imeona mashtaka hayo ni batili, mashtaka hayo yanakufa ndio maana Mahakama ikaamuru marekebisho, hivyo watakata rufaa.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi leo hakimu atakapotoa uamuzi kama anaridhika na ombi la upande wa utetezi ama la. Mbali na Mbowe wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo namba 112 ya 2018 ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu makatibu wakuu Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara).

Wengine ni mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Kawe, Halima Mdee na mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 12 katika kesi ya jinai namba 112 ya mwaka 2018 ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria na kuendelea kufanya mikusanyiko isio halali ama maandamano yaliyosababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Awali, Kibatala aliomba mashtaka yanayowakabili washtaki hao yafutwe kwa kuwa shtaka la nne, latano, la sita na la saba maelezo ya mashtaka hayo yanawachanganya washtakiwa na hawawezi kujitetea kikamilifu. Pia mashtaka hayo kufunguliwa kwake kunahitaji ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambayo haipo.

Alidai kuwa kwa ujumla mapingamizi yake yanaishambulia hati ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao na kwamba mapingamizi hayo ni mapingamizi ya kisheria.

Akiwasilisha mapingamizi hayo, Wakili Kibatala alidai kuwa kibali kilichotolewa na DPP kuipa ridhaa mahakama ya Kisutu kuisikiliza kesi hiyo kina upungufu kwa sababu haisemi imetolewa kwa mashtaka yapi na kwamba imetaja majina ya washtakiwa bila kufafanua makosa waliyotenda.

“Siyo kazi ya mahakama kutafuta mashtaka yanayohusiana na hicho kibali cha DPP, hivyo hoja yetu hakuna ridhaa ya DPP kwa sababu kibali hicho siyo sahihi.” alieleza Kibatala.

“Kwa kuwa shtaka la nne, tano,sita na saba kufunguliwa kwake kunahitaji ridhaa ya DPP, kwa kuwa haipo tunaomba yafutiliwe mbali. Alidai Kibatala.

Pia alidai kuwa hati ya mashtaka inamapungufu kwa sababu shtaka la pili na la Tatu hayana Maelezo ya kutosheleza ya kuwapa msingi na uwezo washtakiwa kujitetea kikamilifu kijinai.

Alidai kuwa katika shtaka la kufanya mkusanyiko bila kibali alijawataja hata watu waliotishiwa na kwamba wametajwa kwa wingi hivyo aijulikani ni washtakiwa ama ni watu wengine.

Kibatala alisema katika pingamizi lingine kuwa mashtaka yanayowakabili wateja wake yamejichanganya hayaonyeshi walipelekeaje kifo cha Akwilina na hao majeruhi walijeruhiwa walijeruhiwa na nani na kwa kutumia nini.

“Maelezo ya shtaka yamerundika vitu vingi kiasi kwamba ni vigumu mtu kujitetea na unapomshtaki mtu kwa kusababisha kifo ni lazima utoe maelezo ya kutosha kuonyesha unamaanisha kitu fulani ili mtu aweze kujitetea.” alieleza Kibatala.

Alidai kuwa hati hiyo ina upungufu kwa kuwa haionyeshi dhumuni la pamoja ambalo washtakiwa walikutana kulitenda hivyo linawanyang’anya washtakiwa haki ya kujitetea.

Kibatala alisema hati ya mashtaka ina upungufu kwa sababu vifungu vilivyotajwa katika shtaka la tatu, tano na saba sio sahihi.

Alidai kuwa katika shtaka la kumi, kumi na moja na kumi na mbili yana upungufu wa kisheria kwa sababu hayaonyeshi watu waliochochewa kufanya makosa ni akina nani waliohudhuria mkutano, wakazi wa kinondoni ama wapiga kura bila kujali itikadi zao.

Baada ya kuwasilisha mapingamizi hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi aliiambia mahakama kuwa wanapinga mapingamizi yote yaliyowasilishwa na upande wa utetezi na kuomba mahakama iyatupilie mbali.

Kuhusu kibali cha DPP kinachoipa mahakama ridhaa ya kusikiliza kesi, Kadushi alidai kuwa hakuna uamuzi wowote ulioweka msingi kwamba ni lazima kiwepo.