Sh600 bilioni kujenga kiwanda cha chuma Dodoma
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa A1 Iron & Steel Tanzania Ltd, Himanshu Tiwari, pamoja na maofisa wa kampuni hiyo na Wizara ya Madini, baada ya mazungumzo kuhusu uwekezaji wa zaidi ya Sh600 bilioni wa kiwanda cha chuma kitakachojengwa eneo la Nala jijini Dodoma.
Muktasari:
- Mradi huo unatarajiwa kutoa ajira 1,500 za moja kwa moja na zaidi ya 5,000 zisizo za moja kwa moja zitakazotokana na shughuli za ujenzi, usafirishaji, huduma, ugavi wa malighafi na uzalishaji wa bidhaa za chuma
Dodoma. Serikali imetangaza kupatikana kwa wawekezaji watakaotekeleza ujenzi wa kiwanda kikubwa cha chuma chenye thamani ya zaidi ya Sh600 bilioni eneo la Nala, jijini Dodoma
Mradi huo utatumia madini ya chuma yanayopatikana nchini, kuzalisha bidhaa mbalimbali za chuma na kuajiri zaidi ya watu 6,500 kwa kazi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Akizungumza jijini Dodoma jana Jumatatu, Juni 15, 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mradi huo utatekelezwa na Kampuni ya A1 Iron & Steel Tanzania Ltd, ukiwa ni matokeo ya mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Tanzania.
Waziri Mavunde amesema Serikali imeweka msisitizo katika uongezaji thamani wa madini ili kuhakikisha rasilimali za nchi hazisafirishwi zikiwa ghafi, bali zinachakatwa ndani ya nchi na kuzalisha bidhaa, ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda.
Amesema mradi huo unakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha madini ya chuma yanachakatwa ndani ya nchi kabla ya kusafirishwa nje.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa A1 Iron & Steel Tanzania Ltd, Himanshu Tiwari, ofisini kwake jijini Dodoma.
“Eneo hili ni la kimkakati na tunasisitiza kukomesha uuzaji wa madini ghafi nje ya nchi,” amesema Mavunde.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kiwanda hicho kitakuwa cha kwanza nchini kuendeshwa kwa mfumo jumuishi wa uzalishaji wa chuma, kuanzia uchakataji wa malighafi hadi bidhaa za mwisho.
Wawekezaji wamesema kiwanda hicho kitatumia teknolojia ya blast furnace na Basic Oxygen Furnace (BOF), mfumo wa kisasa wa uzalishaji unaowezesha chuma kuzalishwa kwa kiwango kikubwa ndani ya viwanda.
Kupitia teknolojia hiyo, kiwanda kitazalisha HR coil, ambayo ni malighafi muhimu katika utengenezaji wa mabati, pamoja na bidhaa nyingine kama steel mesh, binding wire na misumari.
Waziri Mavunde amesema uzalishaji wa bidhaa hizo nchini utapunguza utegemezi wa uagizaji chuma kutoka nje, kushusha gharama kwa watumiaji wa ndani na kuongeza upatikanaji wa vifaa kwa sekta za ujenzi, miundombinu, kilimo, viwanda na madini.
Amesema pia mradi huo utaongeza mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa viwanda kupitia uongezaji thamani wa rasilimali za ndani.
Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa A1 Iron & Steel Tanzania Ltd, Himanshu Tiwari amesema kiwanda hicho kitakuwa cha mfano kwa kuunganisha hatua zote za uzalishaji kuanzia malighafi hadi bidhaa za mwisho.
Mkurugenzi Mtendaji wa A1 Iron & Steel Tanzania Ltd, Himanshu Tiwari, wakati akizungumzia na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde kuhusu mradi huo.
Amesema matumizi ya teknolojia ya blast furnace na BOF yataiwezesha Tanzania kufikia kiwango kikubwa cha uongezaji thamani wa madini ya chuma ndani ya nchi.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kuanza Julai 2026 na kukamilika ndani ya miezi 15.
Mradi huo unatarajiwa kutoa ajira 1,500 za moja kwa moja na zaidi ya 5,000 zisizo za moja kwa moja zitakazotokana na shughuli za ujenzi, usafirishaji, huduma, ugavi wa malighafi na uzalishaji wa bidhaa za chuma.
Serikali imesema itaendelea kuvutia uwekezaji unaounganisha uchimbaji wa madini na uzalishaji wa viwandani, ikisisitiza kuwa huo ndio msingi wa kuongeza thamani ya rasilimali za nchi na kukuza uchumi wa viwanda nchini.