MAAJABU: Kijiji ambacho wanawake, wanaume hutumia lugha tofauti

Muktasari:

Ni vigumu kuwaona wanawake wakizungumzia na wanaume kitu kimoja

Lagos, Nigeria. Najua inaweza kukushangaza, lakini ukweli ndiyo huo kwamba wanawake na wanaume katika kijiji kimoja nchini Nigeria wanazungumza lugha tofauti, yaani wanawake wana lugha yao na wanaume ya kwao.

Kijiji cha Ubang kipo kusini mwa Nigeria ambacho wanaishi jamii ya wakulima wenye utamaduni wa kuzungumza lugha mbili tofauti.

Akiwa amevaa nguo za jadi zenye rangi za kuvutia na kofia nyekundu, Chifu Oliver Ibang aliwaita watoto wake wawili ili kuonyesha mfano mbele ya mwandishi wa Shirika la BBC. Alichukua gimbi, kisha akamuuliza binti yake hiki kinaitwaje? Bintiye alisema bila kusita kinaitwa “irui”. Kisha akamgeukia mwandishi na kumwambia kwamba katika lugha ya kiume gimbi linaitwa “itong.” Pia alitoa mifano zaidi ya maneno. Nguo wanawake huita “nki” na wanaume huita “ariga”.Mbwa wanawake huita “okwakwe” na wanaume huita “abu”

Mti wanawake huita “okweng” na wanaume huita “kitchi” wakati kikombe wanawake hukiita “ogbala” na wanaume huita “nko”

Hiyo ni baadhi ya mifano ya maneno tofauti yanayozungumza na jinsia hizo mbili. Hata hivyo haijulikani hasa kwa nini kuna utofauti baina ya lugha hizi na pengine ni msamiati unaofungamana na tofauti za majukumu ya kiutamaduni kati ya mwanaume na mwanamke.

“Ni kama lugha mbili tofauti,” anasema mtaalamu wa masuala ya kale, Chi Chi Undie. “Kuna maneno mengi ambayo wanaume na wanawake wanachangia, halafu kuna maneno mengine ni tofauti kabisa kulingana na jinsi zao. Hayafanani katika matamshi, hayafanani katika maandishi, yapo tofauti kabisa.” Anasema kwamba tofauti hizo zimekomaa kiasi kwamba haziwezi kuletwa pamoja, kuna tofauti kubwa kuliko hata zile zilizopo baina ya lahaja za Kiingereza cha Uingereza na Marekani. Hata hivyo wanawake na wanaume katika jamii hii wanaelewa kwa usahihi kama sehemu nyingine yoyote duniani.

Chifu Ibang anasema kwamba hupata kazi ya ziada katika kuwafundisha watoto wa kiume lugha wanayopaswa kuzungumza (lugha ya kiume), wakifika umri wanaotakiwa kuzungumza kwani hujikuta wakianza kuzungumza lugha ya kike kwa sababu hutumia muda mwingi wakiwa na mama zao. Mtoto wa kiume anapaswa kuanza kuzungumza lugha ya kiume akitimiza miaka 10.

Chifu anasema kuna hatua ambayo mtoto wa kiume akifika hutambua kuwa lugha anayoizungumza si sahihi na kuanza kubadili bila mtu yeyote kumwambia kuwa anapaswa kuzungumza lugha ya kiume.

Anasema kwa kuanzia huzungumza lugha ya kiume ndipo wanapofahamu kuwa ameanza kupevuka, lakini ikitokea ameshindwa kubadili lugha kutoka ile ya kike kwenda ya kiume, humfikiria kwamba hayuko sawa.

Watu wa jamii ya Ubang wanajivunia utofauti wa lugha yao na wanaona kuwa ndio upekee uliopo baina ya lugha yao na lugha nyingine.

Imeandaliwa na Amani Njoka kwa msaada wa mitandao