Kikongwe wa miaka 87 atupwa jela

Muktasari:

Ni kutokana na kupinga kuwepo mauaji ya Wayahudi wakati wa utawala wa Hitler

Berlin, Ujerumani. Kweli duniani kuna mambo na kama huamini basi tembea uyaone. Mkazi mmoja amehukumiwa kifungo cha miezi minane jela na mahakama moja ya nchini Ujerumani kwa kosa la kukanusha tukio la kuuawa umati wa Wayahudi nchini humo, maarufu kama Holocaust.

Shirika la Habari la Ujerumani limeripoti tukio hilo likisema Ursula Haverbeck, mwenye umri wa miaka 87 alikutwa na hatia ya kukanusha kutokea mauaji hayo na Mahakama ya Detmold imeamua kumfunga jela miezi minane.

Akielezea kile alichokiita msimamo wake, Ursula alisema Wayahudi walikuwa wakiishi maisha salama na ya kawaida katika kambi ya Wanazi ya Auschwitz na kamwe hawakuwa wakiadhibiwa bali hiyo ilikuwa ni kambi ya wafanyakazi wa kawaida tu.

Jaji katika mahakama hiyo aliondoa uwezekano wa kikongwe huyo kupewa msamaha kutokana na historia yake ikiwamo kuonyesha dharau kubwa wakati akiwa mahakamani.

Alisema mtuhumiwa huyo amewahi kukutwa na makosa mengi ambayo baadhi yalichukua sura ya uchochezi.

“Mahakama haitarajii Ursula kupewa msamaha wa parole kwa vile ameonyesha dharau kubwa,” alisema.

Mahakama nyingine zimewahi kutoa hukumu dhidi ya Ursual kutokana na kukanusha mauaji hayo yanayodaiwa kufanywa na Wanazi wa Ujerumani dhidi ya Wayahudi.

Ursula amekuwa akitambulika kutokana na misimamo yake mikali na hivi karibuni alimwandikia barua Meya wa Detmold, Rainer Heller akikanusha kuwapo mauaji hayo ambayo yanadaiwa kufanywa wakati wa utawala wa Adolf Hitler.