Kikosi kazi chaundwa kuzuia 'viroba' toka nje
Muktasari:
Kikosi kazi hicho, mbali na kufuatilia pia kitakuwa na jukumu la kufanya ukaguzi na kitajumuisha Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) , Uhamiaji na Polisi.
Dar es Salaam. Serikali imeunda kikosi kazi cha Taifa cha kufuatilia pombe kali zinazofungashwa kwenye pakiti za plastiki 'viroba' zinazoingia mipakani kutoka nchi za nje.
Kikosi kazi hicho, mbali na kufuatilia pia kitakuwa na jukumu la kufanya ukaguzi na kitajumuisha Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) , Uhamiaji na Polisi.
Akizungumza na wanahabari (leo Jumatatu mchana), Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira, January Makamba amesema lengo la kuunda kikosi kazi hicho ni kudhibiti 'viroba' vinavyoingizwa nchini .
Amesema Serikali imeshatangazwa kupiga marufuku 'viroba' ifikapo Machi Mosi, mwaka huu hivyo mkakati huo lazima uende sambamba na kuzuia viroba vinavyotoka nje ya nchi.
"Doria za ukaguzi wa utekelezaji wa hatua hizi, utaanza wakati wowote kuanzia sasa na hatua kali zitachukuliwa kwa wale wataobainika kukiuka,"amesema Makamba.