Wazazi, wanafunzi waingia taharuki madai ya chakula kuwekwa sumu

Muktasari:

  • Mzazi amekiri kutuma picha kwenye kundi la WhatsApp la wafanyakazi wenzake

Geita. Wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Emaco Vision ya mjini Geita wamepatwa taharuki baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuna mwanafunzi alikusudia kuwawekea wenzake sumu kwenye chakula.

Hata hivyo, taarifa hizo zilikanushwa na uongozi wa shule ambao umelaani kitendo hicho.

Mwanafunzi wa darasa la nne (jina linahifadhiwa) akizungumza na MCL Digital leo Julai 22, 2018 amesema alichanganya maji na majivu kwa ajili ya kucheza na mdogo wake wanayesoma darasa moja.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Octavian Laurian amesema Julai 20, 2018 wakati wa chakula cha mchana kuna mwanafunzi wa darasa la nne alidai mwenzake ana sumu.

Amesema walimu walipochunguza walibaini ni maji machafu yaliyokuwa kwenye chupa.

Laurian amesema kutokana na taharuki iliyokuwapo, uongozi wa shule uliwaita wazazi wa wanafunzi hao wawili na kuzungumza nao.

Amesema jambo la kusikitisha ni kuwa mzazi mmoja alisambaza picha kwenye mtandao na kuzua taharuki kwa wazazi wengine na jamii kwa jumla.

“Watoto walikwenda kuchukua chakula wakiwa kwenye usimamizi wa walimu, walipokuwa wanakula mmoja alikuwa na chupa ndogo yenye maji, wanafunzi wenzake wakawa wamemzunguka na mwalimu alipoona aliwafuta kujua kulikoni mmoja alidai mwenzake ana sumu,” amesema.

Mwalimu Laurian amesema, “Kutokana na kauli ya mtoto, mwalimu aliwachukua na kuwaleta kwa uongozi. Ilibidi tuwaite wazazi tukae nao kwa kuwa maneno hayo ni mazito na hii si mara ya kwanza.”

Amesema walijadili mienendo ya watoto hao na kushauri wazazi kushirikiana na walimu katika malezi.

Kutokana na taarifa kusambaa mitandaoni, amesema walikwenda kutoa taarifa polisi ambazo ziliwezesha kupatikana kwa mzazi aliyezisambaza ambaye baada ya mazungumzo waliridhia kusameheana licha ya kuchafua jina la shule na la mwanafunzi anayetuhumiwa kuwawekea wenzake sumu.

Lidia Charles, mzazi wa mtoto anayedaiwa kuweka sumu kwenye chakula amesema anasikitishwa na kitendo cha picha za mwanaye kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwa kuwa kimesababisha aonekane mbaya na kuzua hofu kwa jamii.

“Nimeumia sana, mwanangu ni mdogo leo anaingizwa kwenye mambo ya uchawi na sumu hili linamuathiri mtoto na limechafua jina la shule,” amesema.

Mzazi mwingine, James Leonard amekiri kutuma picha kwenye kundi la WhatsApp la wafanyakazi wenzake.

Amesema maneno yaliyoko kwenye picha hiyo si ya kwake. Amesema wazazi, uongozi wa shule na polisi wamekubaliana kumaliza tatizo hilo na kuwataka wazazi kutokuwa na hofu.