Afrika yalaani shambulio la kemikali nchini Syria

Muktasari:

  • Pia, Mwenyekiti wa Tume ya AU Moussa Faki ametoa wito wajumbe wa Baraza la Usalama la UN wajadili amani ya Syria

Addis Ababa, Ethiopia. Umoja wa Afrika (AU) umetoa taarifa nzito ya kulaani matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria na umeonya dhidi ya uchukuaji hatua za kujibu bila “kuwa na ushahidi usiokanushika” na iwe kwa kulingana na sheria za kimataifa.

Marekani, Uingereza na Ufaransa zilianzisha mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa ya serikali ya Syria alfajiri ya Jumamosi kujibu kile kinachosadikiwa na majeshi ya Syria kutumia silaha zake kali kwenye maeneo yanayokaliwa na wapinzani na kusababisha vifo vya makumi ya watu wiki iliyopita.

Mwenyekiti wa Tume ya AU, Moussa Faki, alisambaza taarifa hiyo rasmi inayoonyesha msimamo wa bara la Afrika, kwa njia ya Twitter.

Taarifa hiyo iliwataka wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuweka kando tofauti zao na kutafuta amani ya kimataifa.

“Katika mazingira haya magumu, suala pekee linalopaswa kutekelezwa ni kuzidisha juhudi za kimataifa kutafuta suluhisho la kudumu la kisiasa kwa kuzingatia maslahi ya watu wa Syria na kuheshimu mipaka ya taifa la Syria,” alisema.

Taarifa ya AU imetolewa baada ya Algeria kueleza ‘kusikitishwa na mashambulizi kutoka angani’ na pia Misri kulaani matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria.

OPCW yatuma wachunguzi

Shirika la Kimataifa la Udhibiti wa Silaha za Kemikali (OPCW) limesema timu yake ya kutafuta ukweli imewasili Syria lakini ilizuiwa kufika katika eneo linalodaiwa kushambuliwa kwa gesi nchini Syria.

Wachunguzi hao wataanza kazi hiyo leo baada ya Urusi kuridhia. Awali walikuwa wamezuiwa.

Wanatarajiwa kuchukua mchanga na sampuli kusaidia kutambua kemikali zilizotumika katika shambulio hilo.

Mjumbe wa Marekani katika shirika la OPCW hata hivyo ameonyesha wasiwasi wake kwamba Urusi ilitembelea eneo hilo na huenda iliharibu ushahidi ili kuzuia uchunguzi.

Lakini katika mahojiano na BBC, Waziri wa Mambo ya Nje nchini humo, Sergei Lavrov alisema Urusi haijaharibu ushahidi wowote katika eneo hilo.

Alisema kuwa ushahidi uliodaiwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa ulitokana na habari za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na kwamba ushahidi kama huo ni kitu kilichopangwa.

Kauli za May, Macron

Shambulio hilo lilisababisha wimbi la mashambulizi ya mataifa ya Magharibi, wakati wachunguzi wake wakichunguza shambulio hilo karibu na Damascus.

Wakati uchunguzi ukianza, hatua zilizochukuliwa na muungano ulioongozwa na Marekani zinazidi kuleta mitikisiko, huku Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron akidai kwamba amemshawishi Rais Donald Trump kubakisha vikosi vya jeshi la Marekani nchini Syria.

Mjini London, Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May alitarajiwa kujibu maswali katika kikao cha bunge kilichoitishwa kwa dharura jana kuhusiana na kuiingiza nchi yake katika operesheni hiyo.

Operesheni iliyofanywa na nchi hizo ilikuwa ikijibu shambulio la silaha za kemikali iliyotekelezwa na Serikali ya Syria na kulenga raia na kuwaua makumi ya watu.