Irungu akimbizwa hospitalini kwa matibabu

Muktasari:

  • Watu waliomuona walisema kwamba Jowie alikuwa amevaa sare za magereza za rangi ya kijivu. Haikuweza kufahamika mara moja ni kitu gani kilichosababisha maofisa katika gereza anakoshikiliwa kumpeleka hospitalini.

Nairobi, Kenya. Joseph Irungu, mtuhumiwa namba moja katika mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani, Jumatatu alitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta kabla ya kurejeshwa kwenye gereza lililoko eneo la viwanda anakoshikiliwa.
Habari zinasema, kijana huyo maarufu kama Jowie alipelekwa hospitalini akiwa chini ya ulinzi mkali na baadaye alionekana akitembea kwenye vibaraza vya hospitali hiyo.
Watu waliomuona walisema kwamba Jowie alikuwa amevaa sare za magereza za rangi ya kijivu. Haikuweza kufahamika mara moja ni kitu gani kilichosababisha maofisa katika gereza anakoshikiliwa kumpeleka hospitalini.
Oktoba 9, Jowie aliiomba mahakama kumwachia kwa dhamana ili akapate matibabu katika jeraha la risasi lililopo bega la kushoto.
Watu wengine wanaoshukiwa kuhusika au kufahamu mauaji hayo akiwemo mpenzi wake Jacque Maribe waliachiwa kwa dhamana.