Malkia wa muziki wa soul, Aretha Franklin afariki dunia

Muktasari:

Msemaji wa mwanamuziki huyo amethibitisha kuwa Aretha aliyekuwa na umri wa miaka 76 amefariki dunia nyumbani kwake katika jiji la Detroit saa 3:50 asubuhi.

Aretha Franklin, malkia wa muda mrefu wa muziki wa soul amefariki dunia leo Alhamisi Agosti 16, 2018  baada ya kuugua saratani ya kongosho.

Msemaji wa mwanamuziki huyo amethibitisha kuwa Aretha aliyekuwa na umri wa miaka 76 amefariki dunia nyumbani kwake katika jiji la Detroit saa 3:50 asubuhi.

Taarifa ya familia inasema, “tupo  katika wakati mgumu kuliko wote tuliowahi kuwa maishani, tumepoteza nguzo ya familia.”

Mwanamuziki huyo aligundulika kuwa na saratani mwaka 2010 na mwishoni mwa mwaka jana alitangaza kustaafu muziki ili kuongeza nguvu katika matibabu yake.

Onyesho lake la mwisho alifanya Novemba, 2017 katika tamasha lililoandaliwa na mwanamuziki Elton John kwaajili ya kuchangia mfuko wa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.

Akijulikana kwa nyimbo kama Think na Respect, Aretha ni mwanamke mweusi aliyeweka rekodi ya kuwa na nyimbo zaidi ya 20 zilizowahi kushika namba moja katika chati za muziki nchini Marekani.