Marekani, China zajibizana nyongeza ya ushuru

Muktasari:

  • Jumatatu, utawala wa Rais Trump ulitangaza awamu ya tatu na kubwa zaidi ya nyongeza ya ushuru wa forodha kwa bidhaa za China ambao utaanza kufanya kazi Septemba 24 mwaka huu.

Beijing, China. Siku moja baada ya Marekani kutangaza nyongeza ya ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka China, Jumanne China ilitangaza kuchukua “hatua mbadala” dhidi ya uamuzi wa Rais Donald Trump unaolenga kupata mabilioni ya dola huku makundi ya wafanyabiashara yakionya.
Jumatatu, utawala wa Rais Trump ulitangaza awamu ya tatu na kubwa zaidi ya nyongeza ya ushuru wa forodha kwa bidhaa za China ambao utaanza kufanya kazi Septemba 24 mwaka huu.
Katika awamu hii kwanza itaweka nyongeza kwa asilimia 10 kwa bidhaa za China zinazoingizwa Marekani zenye thamani ya dola za Marekani 200 bilioni. Nyongeza hiyo itaongezeka hadi asilimia 25 katika siku zijazo.
Lakini Waziri wa Biashara wa China alitoa taarifa ya kulipa kisasi bali hakutoa maelezo ya kina juu ya uwezekano wa hatua za kuchukua dhidi ya ushuru ulioongezwa na Marekani katika juhudi za mataifa mawili hayo yenye uchumi mkubwa duniani juu ya sera ya teknolojia ya China.
Mapema mwaka huu, Marekani iliweka nyongeza ya ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka China zenye thamani ya dola bilioni 50i.
Hatua hiyo ya hivi karibuni inamaanisha kuwa karibu nusu ya bidhaa zote kutoka China zitawekewa nyongeza ya ushuru wa forodha.
Tofauti na awamu ya kwanza na ya pili ya ushuru wa forodha ambapo uliwekwa hasa katika bidhaa za viwandani na teknolojia, ushuru wa forodha wa hivi karibuni utawekwa katika uwanda mpana wa bidhaa, ikiwemo bidhaa za mlaji. Hiyo inaweza kusababisha kupanda kwa bei kutakapowaathiri walaji wa Marekani.
China nayo ilijibu kwa kuweka ushuru wa forodha. Wakati huu inatarajiwa kuweka ushuru wa forodha kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya dola bilioni 60, ikiwemo gesi asilia iliyo katika hali ya kimiminika.