Rais Ufilipino atishia kuua polisi wanaochunguzwa

Rais Rodrigo Duterte

Muktasari:

Majina ya maofisa wengi wa polisi waliopelekwa kwa Duterte yako chini ya uchunguzi kwa makosa makubwa ya uhalifu yakiwemo ya ubakaji, kuteka, kupotosha na kujihusisha katika biashara ya dawa za kulevya.

Manila, Ufilipino. Rais Rodrigo Duterte ametishia kuwaua makumi ya maofisa wa Jeshi la Polisi la Ufilipino (PNP) ambao wako chini ya uchunguzi kwa uhalifu katika hotuba iliyojaa dharau akilenga wahalifu ndani ya jeshi hilo.
Baada ya kuwapeleka maofisa wa polisi 102 eneo la Malacañang, Duterte, rais mwenye maneno ya ufedhuli, Jumanne aliwashambulia akisema “hawana maana” (na) mzigo kwa jamii.”
Majina ya maofisa wengi wa polisi waliopelekwa kwa Duterte yako chini ya uchunguzi kwa makosa makubwa ya uhalifu yakiwemo ya ubakaji, kuteka, kupotosha na kujihusisha katika biashara ya dawa za kulevya.
Wengine wanalalamikiwa kwa uongozi wa kizembe kama vile kutoweka kazini bila idhini wala likizo na kushindwa kuhudhuria kwenye majukumu ya kimahakama.
Duterte aliwaonya maofisa hao kwamba ikiwa wataendelea na vitendo vyao vya uhalifu itakuwa vema wakiuawa.
"Kama ninyi mfanyavyo, ni rahisi kuua mtu. Ni suala la kumnyatia na kumtwanga risasi mgongoni, kisha unatoweka kimyakimya," alisema.
Vitisho hivyo vilivyofikia kiwango cha juu ni katika juhudi za rais kuhakikisha anaendeleza mtindo wake wa kutia chumvi.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Duterte alitoa wito wa kulifumua jeshi la polisi katika kipindi ambacho mfanyabiashara wa Korea Kusini inadaiwa aliuawa na maofisa wa polisi mafisadi.
"Jisafisheni. Pitieni upya matukio yenu. Nipeni orodha ya maofisa wahuni,” alisema Duterte.