Rais Bongo anasumbuliwa na kiharusi

Muktasari:

  • Makamu wa Rais Pierre Claver Maganga Moussavou amesema Bongo aliugua ugonjwa uitwao CVA (cerebrovascular accident) ambao unafahamika kama kiharusi.

Libreville, Gabon. Rais Ali Bongo, ambaye amekuwa nje ya Gabon tangu alipougua Oktoba akiwa Saudi Arabia, alipata kiharusi, makamu wa rais amesema ikiwa ni taarifa rasmi ya kwanza kuhusu ugonjwa unaomsumbua kiongozi huyo wa nchi.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 59 amelazwa Morocco tangu mapema mwezi huu akitokea Riyadh, Saudi Arabia na kwa sasa anaendelea kupata nafuu katika makazi maalumu jijini Rabat baada ya wiki kadhaa za ukimya juu ya hali yake.
Makamu wa Rais, Pierre Claver Maganga Moussavou amesema Bongo aliugua ugonjwa uitwao CVA (cerebrovascular accident) ambao unafahamika kama kiharusi.
"Tunaomba asiwepo mtu wa kufurahia juu ya kifo au maradhi ya mtu mwingine, na wale ambao hawajui ugonjwa uitwao CVA, waombe Mungu wasimwone yeyote,” Moussavou alisema katika hotuba yake aliyoitoa mjini Franceville, kusini mwa nchi hiyo siku ya Jumamosi.
"Mimi sitamtakia mtu yeyote augue ugonjwa huo, hata adui yangu mkubwa kuliko wote.”
Kukosekana kwa taarifa rasmi baada ya Bongo kuugua alipokwenda kuhudhuria mkutano wa jukwaa la uchumi nchini Saudi Arabia, Oktoba 24, kulichochea uvumi kwamba kiongozi huyo wa Gabon alikuwa dhoofilihali au amefariki dunia.
Makamu wa rais alikuwa sehemu ya ujumbe wa maofisa wa ngazi ya juu waliomtembelea Bongo Jumanne iliyopita nchini Morocco, ambako alisafirishwa mwishoni mwa Novemba baada ya siku kadhaa za matibabu jijini Riyadh.