Spika ailalamikia Serikali kwa kusafirisha binadamu

Muktasari:

  • Kadaga amesema juhudi za Bunge hazijafanikiwa kutokana na maslahi yanayokinzana na maofisa wa ngazi za juu serikalini.

Kampala, Uganda. Spika wa Bunge, Rebecca Kadaga, ameilaumu Serikali kwa kushindwa kupambana na tatizo la usafirishaji wa binadamu.
“Mwaka jana, tuliizuia Serikali kuwaruhusu wanaoitwa wafanyakazi wa ndani kwenda nje. Tulidhani tungewaruhusu wanaotaka kazi kama madereva na wafanyakazi wa mabenki,” amesema Kadaga.
Amesema hayo Alhamisi alipokutana na watawa wa Kikatoliki chini ya mwavuli wao Chama cha Viongozi wa Dini Uganda, ambao walimlalamikia Spika juu ya ongezeko la mateso na utumwa wanaofanyiwa vibarua wa Uganda walioko ughaibuni.
Kadaga amesema juhudi za Bunge hazijafanikiwa kutokana na maslahi yanayokinzana na maofisa wa ngazi za juu serikalini.
“Kwa bahati mbaya, idadi kubwa ya watu serikalini wanamiliki makapuni ya kusafirisha vibarua nje na nimeambiwa wananufaika hivyo lazima iendelezwe,” amesema Kadaga.
Pia amemlaumu Waziri wa Masuala ya Jinsia kwa kuingia makubaliano na nchi zinazopokea vibarua wanaosafirishwa bila Bunge kufahamishwa.