Thursday, August 11, 2016

Trump:Obama, Cliton waanzilishi wa IS

 

Washington, Marekani. Mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Republican, Donald Trump amesema Rais Barack Obama na waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Hillary Clinton ndiyo walioanzisha kundi la kigaidi la Islamic State (IS) hivyo wanaopaswa kulaumiwa.

Trump ambaye amehutubia wafuasi wake katika mji wa Florida akisema  kundi la IS linampa heshima maalumu Rais Obama kwa kuwa ndiye mwanzilishi wake.

Amesema  kuwa Rais Obama na aliyekuwa msaidizi wake katika mambo ya nje ya Marekani,  Clinton ndiyo walioasisi na kuanzisha kundi hilo ambalo limekuwa likiendesha mashambulizi nchini Iraq na Misri.

Katika miezi ya hivi karibuni wafuasi wa kundi hilo wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kushtukiza katika baadhi ya mataifa ya Ulaya na kuua mamia ya watu.

Mgombea huyo wa Republican,   pia amekosoa uamuzi wa Rais Obama kuondoa jeshi Iraq akisema hatua hiyo inatoa nafasi kwa IS kupanua huduma zake duniani.

 Amesema Marekani ilipaswa kubakiza baadhi ya majeshi yake katika ardhi ya Iraq ili kutoruhusu magaidi kudhibiti ardhi ya nchi hiyo.

 

Trump kwa mara nyingine tena ametoa matamshi yanayodhihirisha misimamo yake ya chuki na ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na wageni nchini Marekani.

Trump amedai wakimbizi wa Syria nchini Marekani wanapanga njama ya kufanya shambulizi la kigaidi kama la Septemba 11 mwaka 2011 katika kituo cha biashara cha kimataifa mjini Washington.

Trump alidai lazima Marekani itashuhudia mashambulizi mengine ya kigaidi kama hilo kutoka kwa wakimbizi wa Syria wanaopewa hifadhi katika nchi yao.

“Mambo mengi mabaya yatafanyika nchini, sina shaka kwamba mashambulizi mengi ya kigaidi yatafanyika,yote haya yatasababishwa na kuruhusu wakimbizi wa Syria kumiminika katika nchi yetu,” alisema.

Trump ambaye amekuwa akikosoa siasa za kigeni za nchi hiyo na kuziita  kama msiba kwa sababu zimekosa  mwelekeo alidai  wakimbizi hao hawafai kuruhusiwa Marekani kwani  ni wanaiweka katika hatari ya kukumbwa na shambulizi jingine kama la Septemba 11 lililouwa zaidi ya watu 3,000.

Wachambuzi wa siasa za Marekani na baadhi ya wanachama wa Republican wamekuwa wakikosoa matamshi ya chuki na kibaguzi ya Trump na kusisitiza siyo tu kuwa yanahatarisha usalama wa Marekani bali  dunia nzima.

 Mwanasiasa huyo bilionea pia amekuwa akitoa kauli za chuki dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika na kudai atajenga ukuta ili kuwazua wahamiaji wa Mexico kuingia nchini Marekani.

Juzi, baadhi ya viongozi waandamizi wa Republican waliandika barua ya wazi wakimkosoa Trump kwa kuwa hafai kuwa rais wa Marekani kwa vile ni mlopokaji.

Walisema kuwa Marekani inaweza kuingia katika historia ya ajabu iwapo mwanasiasa huyo atachaguliwa katika uchaguzi wa Novemba.

 

 

-->