Wakuu wa Korea mbili wakutana Pyongyang

Muktasari:

  • Mkutano huo wa viongozi wakuu unakuja wakati kukiwa na mkwamo wa mazungumzo ya kuondokana na silaha za nyuklia kati ya Korea Kaskazini na Marekani.

Pyongyang, Korea Kaskazini. Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in amefanya ziara nyingine katika nchi jirani ya Korea Kaskazini ambako alikutana na kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un kuendeleza mazungumzo kuhusu kuachana kabisa na mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia.
Mbali ya wakuu hao wa nchi kuzungumzia mpango wa kuachana na utengenezaji silaha za nyuklia pia walitarajiwa kujadili suala la kuimarisha uhusiano wake na Marekani.
Baada ya kuwasili na kupokewa kwa shangwe, Rais Moon alitembezwa katikati ya jiji la Pyongyang na kusalimiwa na maelfu ya wananchi waliojitokeza kwa wingi kumwona.
Mkutano huo wa viongozi wakuu unakuja wakati kukiwa na mkwamo wa mazungumzo ya kuondokana na silaha za nyuklia kati ya Korea Kaskazini na Marekani.
Kumekuwa na ushahidi kwamba Korea Kaskazini bado inaendeleza mipango yake ya silaha za nyuklia wakati Marekani inashinikiza Korea Kaskazini ichukue hatua madhubuti za kumaliza mipango hiyo ikiwa ni pamoja na kubainisha silaha na vituo vyake vya silaha za nyuklia.
Korea Kaskazini inasisitiza kuwa kabla ya hilo kufanyika, ni lazima ipate azimio rasmi la kumalizika kwa Vita vya Korea pamoja na kulegezwa kwa vikwazo vya kiuchumi.
Katika ziara hiyo ya siku tatu, Moon anatarajiwa kusaidia kupunguza hali ya wasiwasi wa kijeshi kati ya nchi hizo za Korea na kuunga mkono majadiliano kati ya Marekani na Korea Kaskazini.