Gharama za korosho zazidi

Muktasari:

Ripoti ya wataalam inaonyesha gharama hizo zimeongezeka kutokana na majadiliano ya pamoja ya wizara za kisekta na viongozi wa mikoa na kukubaliana Bodi  ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko iongeze malipo ya gunia (Sh52.50 na gharama ya mwendesha ghala (Sh38.00).

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kununua korosho za wakulima kwa Sh3,300 kwa kilo, imeonekana kuna gharama zinazoongezeka na kufanya ununuzi huo kufikia Sh3,633 kwa kilo kwa mujibu wa ripoti ya timu ya pamoja ya wataalamu kuhusu utekelezaji wa Operesheni Korosho Novemba 27.

Operesheni hiyo ya korosho imekuja baada ya mfumo wa kawaida wa uuzwaji wa korosho kupitia minada kushindikana kutokana na bei ndogo iliyotolewa na wafanyabiashara.

Katika kuweka mambo sawa Serikali iliwasimamisha kazi Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Profesa Wakuru Magigi na kuamua kununua korosho zote kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB).

Bodi hiyo inashirikiana na taasisi nyingine ikiwamo Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Bodi ya Korosho (CBT), Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) na Bodi ya Leseni.

Tangu Serikali ilipoamua kuwalipa wakulima bei hiyo bila kukatwa makato mengine, kumekuwa na maswali mengi kutoka kwa wadau vikiwamo vyama vya ushirika kuhusu gharama za uendeshaji, huku Waziri wa Kilimo Japheth Hasunga akisema kipaumbele ni kumlipa mkulima kisha wataangalia jinsi ya kurudisha gharama hizo.

Akizungumza kwa simu jana, Waziri Hasunga alisema takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuna vyama vya ushirkika 398 na fedha iliyokwenda benki kuwalipa wakulima ni Sh206.9 bilioni na zilizoingizwa kwenye akaunti ni Sh187.4 bilioni. Alisema ripoti ya wataalam imeonyesha gharama zilizoongezeka zimetokana na majadiliano ya pamoja ya wizara za kisekta na viongozi wa mikoa na kukubaliana Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) iongeze malipo ya gunia (Sh52.50) na gharama ya mwendesha ghala (Sh38.00).

“Katika utekelezaji, kumetokea changamoto za malalamiko ya gharama nyingine ambazo hapo mwanzo zilikuwa zinalipwa na mkulima na nyingine zikilipwa na mnunuzi,” imesema ripoti hiyo.