Zitto asema akiwa rais watu watafanya kazi na kula bata

Muktasari:

  • Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo  Zitto Kabwe jana aliweka bayana ndoto zake za kuwania urais baada ya mwaka 2015 kushindwa kufanya hivyo kutokana na umri wa kugombea kutakiwa kuwa miaka 40 na ameahidi akiwa rais watanzania watafanya kazi na kula bata.

Dar es Salaam. Kuna watu wamekuwa wakiishi kwenye ndoto, wapo wanaotamani kuwa madaktari, wapo waliotamani kuwa wachezaji, lakini Zitto Kabwe anawazia urais, na haishii hapo, bali anaeleza hali itakavyokuwa atakaposhika nafasi hiyo ya juu kisiasa.

Zitto ambaye ni kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo jana aliweka bayana ndoto zake za kuwania urais baada ya mwaka 2015 kushindwa kufanya hivyo kutokana na umri wa kugombea kutakiwa kuwa miaka 40.

“(Wananchi) Mtachapa kazi, lakini mtakula bata (mtastarehe),” alindika Zitto.

“Ninaamini nitakuwa rais bora kwa uwezo wake Mola. Nitauona upinzani kama chachu ya maendeleo badala ya kuwa na hofu nao,” alisema mbunge huyo wa Kigoma Mjini

“Nitarejesha taswira chanya ya nchi yetu mbele ya jamii ya kimataifa kwa kulinda demokrasia na haki za binadamu. Mtachapa kazi, Lakini pia mtakula bata,” alisema mwanasiasa huyo kijana

Hakuishi hapo, alisema katika uongozi wake, atamteua Fatma Karume ambaye sasa ni rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kumsaidia kwenye mabadiliko ya mfumo wa utoaji haki.

“Nitamteua @fatma_karume kusimamia mabadiliko makubwa ya mfumo wa utoaji haki nchini ili kukomesha vitendo vya uonevu na ukatili,” amesema.

“Kwa matendo ya nyuma tutaunda Tume ya Ukweli na Maidhiano ili wahanga wajitokeze kwa uwazi na wahusika wa matendo haya wahukumiwe na umma #KaziNaBata,” alisema

Fatma Karume hakuwa mbali na kuitikia wito huo kwa kumjibu Zitto akisema, “@zittokabwe Kazi ya ku-chair (kuwa mwenyekiti wa) Tume ya ku-investigate (kuchunguza) na kutoa mapendekezo ya kubadilisha mfumo wa utoaji haki including namna ya kuwachagua watoa haki; fundamentals ya utoaji haki ni is a job I would truly relish. And I thank you for considering me for that job (ni kazi ambayo ningeifurahia na nakushukuru kwa kufikiria kunipa nafasi hiyo).”

Mara kadhaa Zito amekuwa akizungumzia ndoto zake za kushika nafasi ya juu ya kisiasa nchini licha ya kupitia matatizo kadhaa na amekuwa akieleza ataweza kufanikiwa kama ilivyokuwa kwa waziri mkuu wa zamani wa India, Indira Gandhi.

Na leo alipata nafasi ya kuulizwa maswali kuhusu urais wake ujao.

Mmoja wa wanaomfuata kwenye akaunti hiyo, Magembe Herrera akamuuliza kuhusu ‘fao la kujitoa’, moja ya mambo yanayojadiliwa sana baada ya Serikali kutangaza kanuni za mifuko ya jamii.

“Kuhusu fao la kujitoa kwa tunaofanya kazi za mikataba na mafao ya uzeeni je?” amehoji Herrera.

Mchangiaji mwingine katika hoja hiyo, Frank J Masemele akamgeuzia kibao.

“Acha uongo wewe. Wachapakazi hawana muda wa kula bata. Chagua moja, bata ama kazi. Halafu ndoto zako bwana. Dah,” ameandika Masemele.

Na Zitto hakumuacha.

“Wewe labda! Watanzania wamechoka wanataka #KaziNaBata,” alisema Zitto.