Bavicha wawatembelea Mbowe na Matiko Gerezani

Muktasari:

  • Baraza la vijana chadema (Bavicha) wakiongozwa na mwenyekiti Patrick Olesosop na mwenezi Edward Simbeye wamefika katika gereza la Segerea kwaajili ya kumwona mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe na Ester   Matiko waliofutiwa dhamana.

Dar es Salaam. Baraza la vijana chadema (Bavicha) wakiongozwa na mwenyekiti Patrick Olesosop na mwenezi Edward Simbeye wamefika katika gereza la Segerea kwaajili ya kumwona mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe na Ester   Matiko waliofutiwa dhamana.

Bavicha walifika Segerea majira ya saa nne ikiwa ni utekelezaji wa hadi yao ambayo waliitoa juzi Desemba 8 ambapo Mwenyekiti wao  Patrick Ole Sosopi alisema kufuatia kuahirishwa kwa sherehe za Uhuru, wamepanga kutembelea magereza mbalimbali nchini ili kuzungumza na wafungwa na mahabusu.

Sosopi alisema wameamua kufanya hivyo baada ya Serikali kutangaza kuahirishwa kwa sherehe za miaka 57 ya Uhuru, ambapo fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya shamrashamra hizo zitatumika kujengea Hospitali ya Uhuru jijini Dodoma.

Alisema katika ziara yao magerezani itabeba ujumbe wa hali ya mambo ilivyo nchini kwa sasa.

 “Tunawaomba Desemba 9 iwe siku muhimu sana kuwatembelea mahabusu na wafungwa,” alisema. Katika hatua nyingine, alilaani nguvu inayotumiwa na Jeshi la Polisi wakati wa usikilizwaji wa kesi zinazowakabili viongozi wa chama hicho.