CCM waomboleza kifo cha Mzee Ndejembi

Muktasari:

  • Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Pancras Ndejembi amefariki dunia leo Jumamosi Desemba 29, 2018 katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitamuenzi marehemu Mzee Pancras Ndejembi kwa uwezo wake mkubwa aliokuwa nao katika usuluhishi wa migogoro na mpenda amani katika kipindi cha uhai wake.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Desemba 29, 2018 na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole imesema chama hicho kimepokea kwa mshtuko taarifa za kifo cha kada huyo na kiongozi mstaafu wa chama na Serikali.

“Chama kimepokea kwa mshtuko na huzuni kifo cha Mzee Ndejembi aliyekuwa sehemu ya wazee maarufu na wanaoheshimika katika chama.”

“Chama kilimtumia sana katika kampeni za uchaguzi hasa za urais, hata katika kuleta suluhu na kuimarisha umoja miongoni mwa wanachama, makada na viongozi,” amesema Polepole.

Amesema Mzee Ndejembi ni mojawapo ya viongozi wa CCM walioishi maisha ya kutosheka, unyenyekevu, waliokinai uongozi na kustaafu kwa heshima.

Polepole amesema marehemu Ndejembi aliwahi kuhudumu kwa muda mrefu katika dhamana ya mkuu wa wilaya mbalimbali nchini huku ndani ya chama akihudumu nafasi ya mwenyekiti wa chama mkoa wa Dodoma.

“Uongozi wa chama chini ya mwenyekiti ambaye ni Rais John Magufuli, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally unatoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wanachama wa CCM hasa kutoka mkoa wa Dodoma na wote walioguswa na msiba,” amesema Polepole.

 

mwisho