Dawasa yasema hadi 2020 Dar es Salaam itakuwa na maji ya uhakika

Muktasari:

Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) imesema imejipanga kuhakikisha hadi mwaka 2020 asilimia 95 ya usambazaji maji katika mkoa wa Dar es Salaam inafikiwa.

Dar es Salaam. Tatizo la uhaba wa maji katika jiji la Dar es Salaam linaendelea kupatiwa ufumbuzi na ifikapo mwaka 2020 asilimia 95 ya jiji hilo litapata huduma ya maji safi na salama.

Hayo yameelezwa leo na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), Cyprian Luhemeja wakati akieleza mafanikio ya mamlaka hiyo leo Ijumaa Novemba 16, 2018 katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano.

Amesema hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kuhakikisha hadi kufikia mwaka huo wateja wapya 300,000 wawe wameunganishwa.

Kufanikisha hilo kilomita za mabomba zitatandazwa kwa ajili ya kusambaza maji katika maeneo mbalimbali.

Luhemeja ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu Dawasa imefanikiwa kuwafikia wateja 298,000 kutoka 100,000 ambao walikuwa wakihudumiwa hapo awali.

“Tumewafikia watu wengi na mipango yetu ni kuhakikisha idadi inaongezeka ili tatizo la maji liwe historia katika mkoa huu,” amesema Luhemeja.

Kuhusu upotevu wa maji, Luhemeja ameeleza katika kipindi cha miaka mitatu umepungua kutoka asilimia 57 hadi 37.

Upande wa makusanyo amesema yameongezeka kutoka wastani wa Sh2.9bilioni kwa mwezi mwaka 2015 hadi Sh10.5 bilioni kwa mwezi kwa mwaka 2018 lengo likiwa ni kukusanya Sh12 bilioni kwa mwezi.