Fastjet yasitisha safari

Muktasari:

  • Huku ndege zake zikilalamikiwa kutofanya safari na abiria kusota viwanja vya ndege, kampuni ya Fastjet imetangaza kusitisha safari za Desemba na Januari 2019 kutokana na sababu za utendaji

Dar es Salaam. Kampuni ya Ndege ya Fastjet Tanzania imesitisha safari zake za Desemba 2018 na Januari 2019  kutokana  na sababu za utendaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 17, 2018, menejimenti ya kampuni hiyo imesema wateja wote watarudishiwa nauli zao Desemba 20 mwaka huu kwa utaratibu uliotumika katika manunuzi ya tiketi.
“Fastjet inaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza. Tunawaomba abiria pamoja na mawakala wa safari za anga kuwasiliana nasi kupitia namba za simu za mkononi (zinatajwa) au barua pepe ili kupata ufafanuzi zaidi,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pia imeagiza kampuni na mashirika mbalimbali yaliyokuwa yanafanya biashara na Fastjet yawasiliane kwa njia ya barua pepe au maofisa husika.