Hoja za CAG zazuia likizo za watendaji mkoa Iringa

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi

Muktasari:

  • Katika kuhakikisha hoja za CAG zinazohusu mapato na matumizi zinapata majibu, mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi amewapa siku 30 watendaji wakuu wa halmashauri tano za mkoa huo kuzijadili hoja hizo na kuweka mikakati ya kuzimaliza ili zifungwe.

     

Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amezuia likizo za watendaji wakuu wa halmashauri tano za mkoa huo huku akiwapatia siku 30 kujibu hoja za ukaguzi zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Wakati Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ina hoja 23 ambazo hazijafungwa, Hapi alisema Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ina hoja 18, Kilolo 16, Mufindi 13 na Mafinga Mji 20.

Aliyasema hayo katika ukumbi wa Veta mjini Iringa jana wakati akifungua kikao chake na watendaji hao kilicholenga kuzijadili hoja hizo na kuweka mikakati ya kuzimaliza ili zifungwe.

“Jambo hili halileti picha nzuri, kwa nini takwimu zetu mbaya na kwa nini hatuzifanyii kazi hoja hizo ambazo baadhi yake ni za miaka ya fedha iliyopita?” alihoji.

Hoja hizo zinahusu mapato na matumizi ya halmashauri na utekelezaji wa miradi na mipango mbalimbali ikiwamo ile inayolenga kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu.

“Likizo zote za kuanzia mwezi huu zimesimamishwa. Hakuna mkurugenzi wa halmashauri au mkuu wa idara atakayepewa likizo, washughulikie mzigo mkubwa wa kujibu hoja zao za ukaguzi.”

Pamoja na watendaji hao, Hapi alisema wakuu wa wilaya nao hawatapewa likizo kwa kuwa wana wajibu wa kusimamia utekelezaji wa agizo lake.

Alisema hatakuwa tayari kuona Waziri Mkuu anatumwa mkoani kwake kushughulikia kazi inayotakiwa kufanywa na watu waliopewa dhamana hiyo.

“Kama mnasubiri waziri mkuu atumwe ili aje yatokee yale yaliyotokea Dar es Salaam hivi karibuni, mie sipo tayari,” alisema akimaanisha yaliyowatokea aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba na Charles Mwijage wa Viwanda na Biashara, waliofukuzwa kazi na Rais John Magufuli.