Hukumu kesi ya kupinga sheria ya habari kutolewa

Muktasari:

Walalamikaji wanadai Sura ya 12 ya Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 inakiuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

Arusha. Kesi  ya kupinga Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 namba 2 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na mashirika matatu yakiongozwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) dhidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatarajiwa kutolewa hukumu hivi karibuni.

Walalamikaji wengine ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) wakipinga sheria hiyo kuwa inaminya uhuru wa habari na imempa Waziri mwenye dhamana ya habari kufanya maamuzi yoyote anayoona yanafaa.

Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), Monica Mugenyi akiongoza jopo la majaji wenzake baada ya mabishano ya kisheria kutoka upande wa waleta maombi Wakili Fulgence Massawe na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Alesia Mbuya amesema mahakama itatoa uamuzi wa shauri hilo hivi karibuni.

Awali Wakili Mbuya amedai walalamikaji hawakua na sababu ya kufungua kesi hiyo katika mahakama  hiyo kwa sababu Tanzania ina mfumo madhubuti wa kisheria na ingeweza kusikiliza na kutoa uamuzi wa haki pia alitaka Mahakama itupilie mbali kesi hiyo kwa kuwa lipo shauri kama hilo Mahakama Kuu Mwanza.

Hoja hiyo ilipingwa na wakili Massawe aliyedai maombi  ya Wakili Mbuya hayana msingi kwa kua  hakuna sheria katika Mahakama ya EACJ inayozuia mlalamikaji kuhitaji kesi husika iwe imekamilika katika mahakama ya nchi mwanachama kwanza na kuwa wateja wake hawana kesi kama hiyo katika Mahakama ya Tanzania.