Kampuni zilivyokwama kununua korosho Tanzania

Muktasari:

Kampuni mbili kutoka India na Kenya zilipanga kununua tani 130,000 za korosho nchini kwa bei kati ya Sh3,800 na 3,500 kwa kila kilo, ripoti rasmi imeeleza


Dar es Salaam. Kampuni mbili kutoka India na Kenya zimekwama kununua tani 130,000 za korosho nchini Tanzania kwa bei kati ya Sh3,800 na 3,500 kwa kila kilo.

Hayo yameelezwa katika ripoti ya kutathmini utekelezaji wa operesheni maalumu ya ununuzi wa korosho inayotekelezwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Kampuni ya Kerera ya India iliomba kununua tani 30,000 ikitenga Dola 1,650 za Marekani  kwa kila kilo ambayo ni sawa na Sh3,800,000

Indopower Solution ya Kenya ilitaka kununua tani 100,000 na kila kilo ingenunua kwa Dola 1,535  za Marekani sawa na Sh3,531,000, ripoti hiyo imeeleza.

Kampuni hizo hazikufanikiwa kununua korosho hizo baada ya Serikali kuchukua uamuzi wa kununua yenyewe baada ya mvutano uliodumu kwa siku kadhaa baina ya wakulima na wanunuzi binafsi.

Kampuni hizo zilikuwa ni kati ya kampuni tisa zilizoonesha nia ya kununua korosho na zilizoweza kuendana na tarehe ya mwisho iliyokuwa imewekwa na serikali kwa kampuni zilizokuwa tayari kujiandikisha katika  Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kulikuwa na kampuni tatu za Kitanzania kwenye orodha ya kampuni zilizokuwa zinataka kununua korosho iliyoonwa na gazeti la The Citizen ambazo zilitaka kununua kati ya tani 500 na 100,000 kwa bei ambayo haikuweza kuainishwa katika taarifa hiyo.

Ripoti hiyo iliandaliwa na timu ya pamoja ya wataalamu kutathmini utekelezaji wa operesheni maalumu ya ununuzi wa korosho inayotekelezwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo inabainisha hatua kadhaa za uzalishaji wa zao la korosho na masuala ya masoko ili kuisaidia kufanya uamuzi wake wa usahihi.