Kanuni mpya za Sheria ya Takwimu zaandaliwa

Mwanasheria wa NBS, Oscar Mangula

Muktasari:

Kinachofanywa na NBS ni kuandaa rasimu ya mabadiliko ya kanuni za sheria hiyo na muda utakapofika wadau watashirikishwa lengo likiwa ni kufanikisha utekelezaji wa vifungu vilivyoongezwa kwenye sheria ya mwaka 2015 ambayo ilibadilishwa mwaka huu na kupitishwa na Bunge.

Dar es Salaam. Baada ya Sheria mpya ya Takwimu kusainiwa na kuanza kutumika tangu Septemba 25, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeanza kuandaa rasimu ya mabadiliko ya kanuni.

Mabadiliko hayo yanakusudia kufanikisha utekelezaji wa vifungu vilivyoongezwa kwenye Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 iliyobadilishwa mwaka huu na kupitishwa na Bunge mapema Juni.

Mwanasheria wa NBS, Oscar Mangula aliliambia Mwananchi jana kuwa sasa kinachofanyika ni maandalizi ya ndani kabla wadau hawajahusishwa pindi itakapokamilika ili watoe maoni yao.

“Kanuni zilizopo zilikuwa ni kwa ajili ya Sheria ya mwaka 2015 ambayo imerekebishwa hivi karibuni. Ni lazima tuwe na kanuni za vifungu vilivyoongezwa,” alisema Mangula.

NBS imetangaza kwenye tovuti yake kwamba inaandaa rasimu ya mabadiliko ya kanuni za sheria hiyo na muda utakapofika, itawashirikisha wadau.

“Mabadiliko ya sheria yaliyofanywa yanakusudia kuweka uratibu mzuri wa ukusanyaji na uchapishaji wa takwimu ili kuepuka mkanganyiko unaoweza kujitokeza,” inasomeka sehemu ya taarifa ya NBS na kuwakaribisha wabia wa maendeleo na wadau wote kuendelea kushirikiana na ofisi hiyo na kuishauria katika masuala ya kitaalamu.

Baadhi ya wadau waliyalalamikia mabadiliko yaliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge huku baadhi ya taasisi za kimataifa zikisema yatakwamisha utekelezaji wa majukumu yao nchini.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika, Dk Hafez Ghanem aliyetembelea nchini wiki iliyopita, alisema amezungumza na Rais John Magufuli na kuiomba Serikali kuangalia namna wadau wanavyoweza kutekeleza majukumu yao kwa uhuru zaidi.

“Benki ya Dunia haiwezi kufanyakazi bila takwimu. Tumeiomba Serikali iangalie jinsi itakavyorahisisha ukusanyaji na uchapaji wa takwimu kutoka vyanzo tofauti kwa matumizi mbalimbali,” alisema Dk Ghanem.