Kitilya na wenzake kula Krismasi ya tatu rumande

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa kampuni ya Egma inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana, Harry Kitilya na maofisa wa zamani wa benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon watamaliza mwaka wa 2018 bila ya shauri lao kuanza kusikilizwa baada ya mahakama kuambiwa jana kuwa upelelezi haujakamilika.

Kitilya, ambaye alikuwa kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Shose, ambaye alikuwa Miss Tanzania wa mwaka 1996 na Sioi, walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza Aprili mosi 2016 na kusomewa mashtaka manane, likiwemo utakatishaji ambalo halina dhamana.

Wakili wa Serikali, Wankyo Saimon alisema jana kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kumuomba Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kupanga tarehe nyingine.

Washtakiwa hao, ambao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha, wamerejeshwa rumande ambakoi wameshaishi kwa takribani miaka miwili sasa tangu wakamatwe.

Hakimu Shaidi alihirisha kesi hiyo hadi Desemba 28, 2018.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola 550 milioni za Kimarekani kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard ya Uingereza.

Wanadaiwa kuwa Machi 2013 jijini Dar es Salaam walijipatia dola 6 milioni, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya kuwezesha kupatikana kwa mkopo na zililipwa kupitia kampuni ya Egma T Ltd.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha fedha kwa kuhamisha, kuchukua na kuweka kiasi cha Dola za Marekani 6 milioni katika akaunti tofauti tofauti za benki.

Kati ya Machi 2013 na Septemba 2015, wanadaiwa kuwa waliweka pesa hizo katika akaunti mbalimbali zinazomilikiwa na kampuni ya Egma na kwamba walipaswa kufahamu kuwa pesa hizo zilitokana na vitendo vya kughushi.