Lowassa afichua siri ya mradi wa maji Ziwa Victoria

Waziri Mkuu aliyejiuzulu  ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa  akiwasalimu waumini wa Kanisa la  Africa Inland  Pastoreti  ya Kahama Shinyanga, alipowasili  wakati wa ibada na harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya msingi ya kanisa hilo  jana. Picha na Mpiga Picha Maalumu. 

Muktasari:

  • Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, aliwataja mawaziri waliounga mkono mradi huo kuwa ni Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Mohamed Seif Khatibu, aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais.

Kahama. Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amefichua siri ya jinsi mpango wa kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria ulivyopingwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri wakati wa utawala wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Akizungumza katika harambee ya kuchangia Shule ya Msingi ya Kanisa la AICT huko Kahama mkoani Shinyanga jana, Lowassa, ambaye katika kipindi hicho alikuwa Waziri wa Maji, alisema mawaziri wawili tu ndio waliunga mkono mradi huo na waliobakia waliupinga. Mradi huo wa maji unapita katika Mikoa ya Mwanza na Shinyanga.

Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, aliwataja mawaziri waliounga mkono mradi huo kuwa ni Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Mohamed Seif Khatibu, aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais.

“Niwapeni siri, nilipendekeza mradi wa kutumia maji ya Ziwa Victoria kwa Rais Mkapa naye akaniuliza wale wakubwa tutawaweza, nikamhakikishia tutawaweza.

“Wakubwa hao alikuwa na maana ya nchi za Misri, Ethiopia na Sudan zinazotumia Mto Nile unaoanzia kwenye Ziwa Victoria.

“Rais Mkapa alitaka mawazo ya kila waziri na mawaziri wawili tu ndio waliunga mkono mradi huu na hao ni Rais Kikwete wakati huo akiwa waziri na rafiki yangu Mohamed Seif Khatibu waliuafiki. Mzee Mkapa baada ya kusikiliza mawazo yote akaamua fedha zitolewe,” alisisitiza.

Lowassa alisema kulikuwa na ugumu kwenye mradi ule wakati mkataba wa zamani wa kimataifa unaipa Misri haki ya kumiliki Ziwa Victoria kwa sababu Mto Nile, ambao ni tegemeo la nchi hiyo, unaanzia hapo.

“Nilikuwa na wakati mgumu wakati ule nilipokwenda Misri maana  wakati nateremka pale Uwanja wa Ndege wa Cairo, nilikuta ulinzi wa hali ya juu sana, nikajiuliza mimi waziri tu napewa ulinzi namna hii.