Lukuvi: Migogoro ya ardhi Tanzania itamalizika mwaka 2020

Muktasari:

Serikali imeahidi kumaliza migogoro yote ya ardhi iliyopo nchini Tanzania kabla mwaka 2020


Babati. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi  amesema atahakikisha migogoro yote ya ardhi nchini Tanzania inamalizika mwaka 2020 kama alivyoagiza Rais John Magufuli.

Lukuvi aliyasema hayo leo Novemba 22, 2018 mjini Babati mkoani Manyara alipotembelea mashamba ya wawekezaji wazawa eneo la Singu na Endasago wenye mgogoro na wananchi.

Amesema atahakikisha anatatua migogoro yote iliyopo Tanzania na ameshawaagiza wakuu wote wa wilaya wamalize migogoro ya ardhi ya vijiji.

"Unakuta kijiji na kijiji wanagombea mpaka bila sababu maalum wakati  wote ni Watanzania. Nimeagiza upimaji wote ufanyike ili kumaliza migogoro hiyo," amesema Lukuvi.

Amesema hivi sasa migogoro mingi ya ardhi imepungua na amejipanga kuhakikisha migogoro hiyo inamalizika kama agizo la Rais Magufuli lilivyotamka.

Aiagiza halmashauri ya wilaya ya Babati na maofisa wa ardhi wa kanda ya kaskazini kupima upya shamba la Endasago lenye mgogoro kati ya mmiliki na wanavijiji wa Endasago na Dudiye.

"Huyu mmiliki wa shamba hilo lenye ekari 1,300 hana hati wala halipi kodi hivyo aombe upya na vipimo vifanyike wananchi waliopo eneo hilo walioishi muda mrefu watakatiwa eneo na halmashauri imege sehemu ya huduma za jamii ikiwemo soko," alisema Lukuvi.

Mmiliki wa shamba hilo Abdilahi Mchinja alikubaliana na uamuzi wa Waziri Lukuvi na aliahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa ajili ya kutekeleza agizo hilo.

Mmiliki wa shamba la Singu, David Bategereza ameagiza shughuli za upimaji viwanja zisitishwe hadi hapo upimaji utakapofanyika upya.

"Nimeagiza yule mpimaji asimame kufanya shughuli hiyo na zoezi la kuweka miundombinu ya nishati ya umeme liendelee, mipaka ya vijiji vinavyozunguka shamba ifufuliwe upya," amesema Lukuvi.

Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul amepongeza Lukuvi kwa uamuzi alioutoa kwani migogoro hiyo ni ya muda mrefu na ilikosa ufumbuzi.

"Wananchi walishindwa kulima kutokana na mgogoro huo na wale waliojenga nyumba walikuwa wanaishi kwa hofu ila leo Waziri umefika na kuzungumza nao," amesema Gekul.