Lukuvi aipiga kufuli Ofisi ya ardhi ya Jiji la Dar

Muktasari:

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amezifunga ofisi za ardhi za jijini Dar es Salaam kwa madai ya kuwa chimbuko la utapeli na ubadhilifu


Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  William Lukuvi amezifunga ofisi za ardhi na masijala za Jiji la Dar es Salaam.

Amechukua hatua hiyo leo Alhamisi Novemba 29, 2018 baada ya kubainika kuwa ofisi hizo ndio chimbuko la utapeli na ubadhilifu wa ardhi jijini humo.

Amesema jiji hilo halina ardhi, halipangi, halipimi na wala halimilikishi lakini bado hadi sasa wanaendelea kutoa ofa za ardhi ambazo zinaisumbua wizara yake, kubainisha kuwa shughuli zote za ardhi zitafanywa na wilaya tano za Dar es Salaam na kanda.

Amesema kwa sasa mtu yeyote mwenye ofa yenye muhuri wa jiji la Dar es Salaam hautatambulika na kuwataka wahusika kwenda katika manispaa kuuliza utaratibu mwingine.

Amesema wakishaingia kwenye mfumo wa kidigitali, ofisi za mikoa za ardhi hazitatambulika tena, kuanzia sasa maombi ya ardhi yatatoka wilayani kwenda kwa kamishna wa ardhi wa wilaya husika.

"Kuna watu wamekaa mkao wa kula kazi yao kuchapisha ofa za jiji, nilishatoa miaka miwili watu kwenye ofa hizi wazibadilishe kupitia kwa maofisa wa ardhi wa wilaya, kuanzia saa imekula kwao,” amesema Lukuvi.

“Tunatoa hati moja kwa moja hakuna ofa, nimeamua kufunga ofisi ya ardhi za jiji na watendaji wote wataripoti wizarani. Mawasiliano yatafanywa na manispaa yatakuja wizarani.”

Amesema kesho wafanyakazi wa ardhi katika ofisi hiyo iliyofungwa wanapaswa kuripoti kwa kamishna wa ardhi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kupangiwa kazi.