Lukuvi atoa miezi miwili wakazi Moshi walipe kodi ya ardhi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi 

Muktasari:

  • Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi  leo Alhamisi ametoa miezi miwili kwa wananchi wa wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro ambao hawana hati na ambao hawajalipa kodi, kuhakikisha wanafuatilia hati zao na kulipa kodi ili kuiwezesha Serikali kupata mapato.

Moshi. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi ametoa miezi miwili kwa wakazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro ambao hawana hati na ambao hawajalipa kodi, kuzifuatilia ili waweze kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.

Lukuvi amesema ifikapo Februari mwaka 2019 kwa wananchi ambao watakuwa hawana hati na hawajalipa kodi, watafikishwa mahakamani.

Akizungumza  katika ukumbi wa Mkoa wa Kilimanjaro leo Alhamisi Novemba 15, 2018 wakati akisikiliza kero za wananchi wa wilaya ya Moshi, amesema Moshi inaongoza kwa kutolipa kodi, hivyo ni lazima sheria na taratibu za ardhi zitekelezwe.

"Namuagiza mwenyekiti wa baraza la ardhi, ifikapo Februari mwakani mtu yeyote ambaye anaishi Moshi, kwenye eneo lililopimwa, aidha kiwanja cha nyumba, kihamba  sijui nini, hana hati, tupambane naye mahakamani," amesema Lukuvi.

"Naagiza ikifika mwezi wa pili, mwenyekiti unasimamisha kesi zote na kusikiliza kesi za hawa ambao hawataki kulipa kodi Moshi, nataka kodi zitozwe kwa asilimia 100, faini zitozwe hata kama ni kuuza nyumba ziuzwe," ameongeza.

Amesema lazima mwezi wa pili waanzishe mahakama maalumu Moshi kudai kodi kwa kuwa uwezo wa kulipa wanao lakini wanalipa chini ya asilimia 50 kwa mwaka.

Amesema kila mwananchi ambaye anaishi eneo lililopangwa, lazima afuate taratibu na  awe na hati mkononi na kwamba wale ambao hawajalipa kodi na wale ambao wameshapimiwa na hawajachukua hati zao Februari wote wasakwe na wapelekwe mahakamani.

"Wapo watu ambao walishapimiwa nawapeni miezi miwili, nendeni manispaa mkaombe hati, kwa ambaye hana hati, afanye jitihada za kuhakikisha anakuwa na hati ili alipe kodi na waendeleze maeneo kwa mujibu wa masharti ya mipango miji"

"Mwezi wa pili tutakuja kufanya ukaguzi, huna hati au una hati na hujalipa kodi tutakupeleka mahakamani, kwani kuna watu 5,000 hawajapewa hati manispaa ya Moshi, wengine kwa udhaifu wao na wengine kwa udhaifu wa manispaa"

Amesema watu ambao hawapendi kuchukua hati ambao hawalipi kodi ni wahujumu uchumi, kwa kuwa wanasababisha Serikali kukosa mapato.

Aidha amesema si hiari ya wananchi wanaoishi mjini kuchukua hati au kulipa, bali ni lazima kwa mujibu wa taratibu za mipango miji, hivyo kwa ambao hawatatekeleza hilo, Serikali itapambana nao.

Waziri huyo amesema uongozi wa Manispaa ya Moshi wana tatizo la kutodai kodi, kutotoa hati na hawajibu barua wanazoandikiwa na wananchi juu ya malalamiko ya ardhi.

Amesema watendaji wa manispaa, hawatendi kwa mujibu wa taratibu na hawawajibiki, na hajui kama wamechoka au wameamua.

Amesema wapo wananchi ambao wamepimiwa maeneo yao hawajapewa hati na wengine wameandika barua kwa zaidi ya miaka 18 lakini hawajajibiwa mpaka sasa.

"Jana nilikuwa ofisi za manispaa ya Moshi, baadhi ya watu wamepimiwa viwanja hawajapewa hati zao, wapo walioandika barua manispaa, hawajibiwi kwa miaka 18, kwenye faili zipo lakini hazisomwi na watendaji wapo pale wanapokea mshahara, utendaji wa maofisa pale Moshi ni sifuri," amesema Lukuvi.

"Manispaa wamekiri wenyewe watu 5,000  hawajapata hati, lakini pia lipo tatizo, hawajibu barua, sijui wamezoeleka sana, nitatafuta sura ambazo hazijazoeleka Moshi nizilete," amesema.

Lukuvi ametumia pia nafasi hiyo, kuagiza manispaa na miji yote kusimamia watu kuishi kwa kufuata sheria za mipango miji na kueleza watu hawawezi kuishi kama wanavyotaka.