Magufuli apiga 8 nzito

Muktasari:

Rais Magufuli amegawa  vitambulisho 675,000 kwa ajili ya kuwatambua wafanyabiashara wadogo nchini Tanzania, asisitiza ukusanyaji kodi

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema haridhishwi na ufanisi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Rais Magufuli amesema licha ya mapato kuongezeka, mamlaka hiyo haizitumii vyema fursa zilizopo nchini, badala yake ina utitiri na inatoza viwango vikubwa vya kodi.

Makusanyo ya mapato yameongezeka kutoka wastani wa Sh800 bilioni mwaka 2014/2015 hadi Sh1.3 trilioni kwa sasa.

Akizungumza jana katika kikao cha kazi cha TRA, mawaziri na wakuu wa mikoa jijini hapa, Rais Magufuli alisema ingawa uchumi umekua kwa wastani mzuri kwa miaka ya hivi karibuni, ukusanyaji wa mapato bado uko chini.

Alisema takwimu zinaonyesha uchumi unakua, lakini kiwango cha ukusanyaji kodi kipo chini ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika, hivyo kuitaka TRA ijitathmini.

“Kuna walipa kodi milioni 2.27 uwiano wa kodi inayokusanywa na Pato la Taifa (GDP) ni asilimia 12.8 kiwango ambacho ni cha chini ukilinganisha na nchi nyingine Afrika. Kwenye suala la ukusanyaji mapato hatufanyi vizuri,” alisema.

Aliitaka TRA kuongeza idadi ya walipakodi badala ya kuongeza wingi na viwango vinavyotozwa kwa walipaji waliopo.

Alitoa mfano wa Afrika Kusini ambayo uwiano wa walipaji na GDP ni asilimia 26 wakati Kenya ni asilimia 18.5 na Msumbiji asilimia 18. Uwiano huo nchini Zambia ni asilimia 15.8 na Uganda ni asilimia 14.2.

“Wigo huu mdogo unatokana na nchi yetu kushindwa kutumia fursa za vyanzo vipya vya mapato vilivyopo. Ikiwa Msumbiji wapo milioni 27 ila wana walipakodi milioni 5.3 inakuwaje sisi tulio milioni 55 tukawa nao milioni 2.2?,” alihoji.

Alisema ufinyu wa makusanyo unatokana na kutorasimishwa kwa biashara hali inayosababisha kukosa vyanzo imara vya mapato.

Ukubwa, wingi wa kodi

Magufuli alisema kuna malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara juu ya viwango vikubwa na wingi wa kodi zilizopo ambazo zimewalazimu wengi kufunga biashara kutokana na kushindwa kuzimudu.

Tathmini ya Wizara ya Fedha na Mipango mpaka Juni 2017 ilionyesha zaidi ya biashara 200,000 zilifungwa kutokana na sababu mbalimbali nchini.

Suala hilo siyo tu limewaathiri wafanyabiashara pekee, bali limeinyima TRA mapato muhimu ya kufanikisha malengo ya Serikali.

Licha ya biashara kufungwa, Rais alilitaja eneo ambalo ufanisi wa TRA upo chini zaidi ni ukusanyaji wa kodi ya majengo akisisitiza kuwa mpaka sasa ni nyumba milioni 1.6 pekee ndizo zimesajiliwa nchini.

“Una ofisi kwenye kila halmashauri nchini, lakini unashindwa kukusanya kodi ya majengo,” alisema Rais.

Mazingira ya biashara

Rais Magufuli alijibu hoja za muda mrefu zilizokuwa zinatolewa na sekta binafsi kwamba kuna changamoto nyingi zinazowakatisha tamaa wawekezaji wa ndani na hata wa nje ya nchi.

Alisema upo ugumu wa ufanyaji biashara unaotokana na urasimu uliopo kwenye mamlaka za usimamizi. “Wafanyabiashara wanahangaika kutoa mizigo yao bandarini na wanacheleweshwa makusudi. TRA na mamlaka nyingine hakikisheni mnatengeneza mazingira rahisi ya watu kulipa kodi kwani tumeshindwa kuvutia uwekezaji.”

Jeshi la Polisi

Pamoja na kadhia zinazosababishwa na watendaji, Rais Magufuli alisema Jeshi la Polisi limekuwa kikwazo kwa wafanyabiashara hasa wasafirishaji wa mizigo nje ya nchi.

“Bado tuna vizuizi barabarani, vilivyo rasmi na visivyo rasmi. Unakuta gari ipo kwenye transit (inasafirisha mizigo kwenda nje ya nchi), lakini mtu anajisikia tu kuisimamisha hata kwa saa sita au saba, baadaye anairuhusu iondoke”

Alisema, “Hii inawakatisha tamaa wafanyabiashara.”

Alilitaka jeshi hilo kusimamia sheria na si kutumia vibaya mamlaka waliyo nayo kukwamisha shughuli za maendeleo. Hata watendaji wake, alisema wapo wanaoshirikiana na wakwepa kodi kujinufaisha na akabainisha kuwa ameshalazimika kuchukua hatua.

“Aliyekuwa RPC wa Kagera nilimtoa kwa sababu alikuwa anawasindikiza wakwepa kodi hadi mpakani kule Mutukula. Nimeagiza achunguzwe,” alisema.

Oktoba 8, Rais Magufuli aliagiza kusimamishwa kazi Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi; Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kyerwa, Justine Joseph; Mkuu wa Upelelezi wa wilaya hiyo, Everist Kivuyo na Mkuu wa Kituo cha Polisi Kyerwa, Robert Marwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuhusika katika magendo ya kahawa na tuhuma nyingine.

Uaminifu TRA

Ingawa Kamishna wa TRA, Charles Kichere alisema wana upungufu wa wafanyakazi 1,930 na magari 250 hivyo kuwapa changamoto kuwafikia wananchi wengi zaidi, Rais alisema kuna watumishi wasio waaminifu ambao hushirikiana na wakwepa kodi.

Alisema wapo watumishi ambao hushiriki kufunga baadhi ya biashara ili kuwaruhusu wamiliki wake kukwepa kodi, ujanja ambao ukibainika wahusika huishia kuhamishwa.

“Kwa kufanya hivi huwa wanahama na mtandao wao. Wakibainika watu kama hawa fukuza.”

Utitiri wa taasisi

Rais alisema zipo baadhi ya taasisi ambazo zilianzishwa kwa ajili ya kukuza uwekezaji, lakini kwa sasa zimegeuka kuwa kikwazo kutokana na kutowajibika ipasavyo. Alisema utitiri wa taasisi hizo umeendelea kuchelewesha kasi ya uwekezaji nchini kutokana na kutofanya kazi kwa ukaribu.

Kwenye orodha hiyo licha ya TRA, alikitaja Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Shirika la Viwango (TBS) kutumia mifumo ya kielektroniki katika kuunganisha huduma zao.

Maduka ya kubadilisha fedha

Awali akitoa taarifa ya utendaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Gavana Frolens Luoga alisema wataendelea kusimamia uendeshaji wa maduka ya kubadilishia fedha na kuyafunga kila inapobidi.

“Udhibiti utaendelea kuwa mkali. Hatuhitaji maduka 100 ya kubadilisha fedha jijini Dar es Salaam, huduma hizo zitapatikana sehemu muhimu kama hoteli za kitalii na benki,” alisema.

Rais alisema uwepo wa maduka mengi ya kubadilishia fedha umesababisha kukithiri kwa vitendo vya utakatishaji fedha ambao ni kikwazo katika uchumi.

“Kuna mtu alikuwa na leseni moja, lakini akafungua matawi mengine saba. Bado fedha anazobadilisha hakuna mapato anayolipa TRA,” alisema Magufuli.

Vitambulisho wamachinga

Ili kuhakikisha biashara ndogo zinarasimishwa, Rais Magufuli alitoa vitambulisho 670,000 vya kuwatambua wafanyabiashara ndogo nchini vitakavyohakikisha hawasumbuliwi. Alimkabidhi kila mkuu wa mkoa vitambulisho 25,000.

Alimtaka kila mkuu wa mkoa kuvigawa kwenye eneo lake kwa malipo ya Sh20,000 kila kimoja na kuagiza vingine kadri mahitaji yatakavyoongezeka. Kila mkoa utakusanya Sh500 milioni hivyo ujumla Sh13 bilioni zitapatikana.

“Usajili wa wafanyabiashara unaenda polepole sana. Unakuta mtu ana mtaji usiozidi Sh4 milioni lakini kila siku anafuatwa alipe kodi na ushuru wa kila aina,” alisema.