Magufuli asema fedha za mkopo mradi wa maji Arusha zitalipwa na Watanzania wote

Rais John Magufuli

Muktasari:

  • Rais John Magufuli amesema Sh520bilioni za mkopo kwa ajili ya mradi wa maji jijini Arusha zitalipwa na Watanzania wote

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Sh520bilioni za mradi wa maji safi na maji taka unaotekelezwa jijini Arusha zitalipwa na Watanzania wote.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Desemba 2, 2018 wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa uboreshaji wa huduma za maji safi na maji taka katika kijiji cha Kimnyaki jijini Arusha.

Amesema kama ilivyokuwa kwa mikopo mingine inavyolipwa na watu kutoka sehemu mbalimbali ndivyo hivyo itakuwa katika kulipa fedha hizo.

"Tena tumezileta katika eneo ambalo nilikuwa natukanwa lakini yote ni kwa sababu maendeleo hayachagui chama wala kabila," amesema.

Amesema maji yanayozalishwa katika eneo hilo ni lazima yawanufaishe watu wote ambao mradi huo utapita ili kuhakikisha kuwa dhana halisi ya mradi mkubwa inazaa matunda.

"Nikupongeze sana waziri hasa kwa kufukuza wakandarasi wanaochelewesha miradi na hata mimi nilipokuwa waziri nilifukuza wengi na waliponiombea laana hazikunipata hivyo nikuombe wanaochelewesha miradi fukuza," amesema.

Mbali na hilo aliishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika ambayo inatoa mikopo isiyo na masharti kama ilivyokuwa kwa benki nyingine ambazo hutoa mikopo isiyokuwa na faida.

"Nimesema katika awamu hii hatutakopa kwa ajili ya mradi wa aina hii bali tutakopa kwa ajili ya miradi itakayoonyesha faida kwa wananchi wa aina zote," amesema.