Majaliwa aagiza uchunguzi fedha za Hospitali Nachingwea

Muktasari:

  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kuundwa timu ya kufuatilia Sh700 milioni zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea na matumizi ya Sh400 milioni zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kilimarondo.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kuundwa timu ya kufuatilia Sh700 milioni zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi ambazo mpaka sasa hakuna kazi iliyofanyika.

Alitoa maagizo hayo jana Jumamosi, Novemba 17, 2018, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Kilimarondo mkoani Lindi.

Pia Waziri Mkuu ameagiza timu hiyo itakayoundwa, ikague matumizi ya Sh400 milioni zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Kilimarondo ambazo mpaka sasa zimeisha huku ujenzi ukiwa bado haujakamilika.

Maagizo hayo yalitokana na mbunge wa Nachingwea (CCM), Hassan Masala kumueleza miradi hiyo miwili licha ya kutengewa fedha na Serikali bado haijakamilika.

“Serikali haitaki mzaha na fedha za umma, hivyo mkuu wa mkoa unda timu ya wataalamu kutoka mkoani waje Nachingwea kufuatilia ni kwa nini fedha zimetolewa tangu Julai ili kukarabati hospitali ya wilaya ziwe hazijatumika hadi leo, pia tujue kama kweli bado zipo,” alisema Majaliwa.

Pia ilielezwa kuwa ili mradi wa ujenzi wa kituo cha afya katika eneo hilo ukamilike inahitajika Sh51 milioni ambapo Waziri mkuu aliitaka Halmashauri ya Nachingwea kuhakikisha fedha hizo zinatolewa,

Kuhusu upatikanaji wa umeme katika eneo hilo, Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kusambaza umeme katika maeneo yote ambayo bado hayajaunganishiwa nishati hiyo nchini yataunganishiwa, ikiwemo na tarafa ya Kilimarondo.

Alisema Rais John Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu. “Serikali imetenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika maeneo yote kwa gharama ya Sh27,000 tu”.

Pia Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kwamba hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.