Majaliwa afungua soko la mazao Songea

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Muktasari:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Alhamisi Januari 3, 2019 ameendelea na ziara yake  ya siku nne mkoani Ruvuma kwa kufungua soko la mazao na kuwahimiza wananchi kutumia mvua zinazoendelea kunyesha nchini Tanzania kulima kwa wingi mazao ya  chakula na biashara

Dar es  Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefungua mradi wa maghala ya kuhifadhi nafaka na soko la mazao la OTC-Lilambo katika Halmashauri ya Songea mkoani Ruvuma lililogharimu Sh1.5bilioni.

 Amesema Rais John Magufuli ameazimia kuwawezesha wakulima kuwa na mahali sehemu ya uhakika ya kuhifadhi mazao yao na sehemu ya kufanya biashara ili kuwaongezea tija.

 Amefungua soko hilo leo Alhamisi Januari 3, 2019 akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku nne ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Ruvuma.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na ofisi ya waziri mkuu leo , imemnukuu akisema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa soko hilo pamoja na maghala kwa kuwa umezingatia viwango.

 Maghala hayo mawili yana uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 za nafaka.

“Licha ya soko hili kuwapa wakulima wetu fursa ya kupata masoko ya kuuzia mazao yao, pia watapata mafunzo ya namna ya kuhifadhi bidhaa zao pamoja na taarifa za masoko,” amesema Majaliwa.

Pia, ameiagiza bodi ya soko hilo kuhakikisha inatoa matangazo katika vyombo mbalimbali vya habari ili wakulima waweze kupeleka mazao yao sokoni hapo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka wananchi kutumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha nchini kwa ajili ya kuandaa mashamba, kupanda mazao ya chakula na biashara.

“Nawaagiza viongozi wa kata na vijiji hakikisheni wananchi katika maeneo yenu wanaandaa mashamba na kupanda kwa wakati, tunataka tuwe na chakula  cha kutosha na ziada tuuze,” amesema

Awali, kaimu mkurugenzi mtendaji wa Wilaya ya Songea, Martin Mtani ameiomba Serikali iwapatie mashine itakayowawezesha kupanga madaraja ya mazao ya nafaka mbalimbali.

Mkurugenzi huyo ameomba soko hilo liwekwe kwenye mpango wa kujengewa vihenge vyenye uwezo wa kukausha mazao kwa viwango vya kimataifa ili kutatua tatizo la unyaufu.

Pia Mkurugenzi huyo ameiomba Serikali iwasaidie kuliunganisha soko hilo na TMX ili waweze kuuza mazao ya nafaka ndani na nje ya nchi .

Ufunguzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Jenister Mhagama na Waziri wa Kilimo,  Japhet Hasunga.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Damas Ndumbaro, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme na maofisa wengine wa Serikali.