Makandarasi kuhakikiwa kabla ya kupewa kazi

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa

Muktasari:

Makandarasi wa miradi ya maji kuhakikiwa kwa kina kabla ya kupewa kazi ili kuondoa mazingira ya kuchukua kampuni zisizokuwa na uwezo.


Bagamoyo. Kusuasua kwa miradi mbalimbali ya maji kunasababishwa na makandarasi kutofanyiwa uhakiki kabla ya kupewa kazi na kutosimamiwa vizuri jambo ambalo Serikali ya Tanzania  imelibaini na imeanza kuwafanyia uhakiki.

Jambo hilo linasababisha miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango na mingine kutokamilika.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne Desemba 18, 2018 na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa katika ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maji wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani.

Amesema kwa kutambua hilo Serikali kabla ya kutoa kandarasi inafanya uhakiki wa kina kwa kampuni husika na kujua taarifa zake zote ikiwemo kupitia kazi alizofanya.

“Hilo tumeshalianza tunahakiki mkandarasi kwa kina kabla ya kumpa kazi maana changamoto hii imekuwa ikitusumbua kwa muda mrefu,” amesema Mbarawa.

Kuhusu usimamizi wa miradi, Profesa Mbarawa amewataka watumishi wa mamlaka za maji wanaopewa dhamana hiyo kufanya kazi kwa uaminifu.

“Lazima tuwe wazalendo, ukipewa jukumu la kusimamia mradi tanguliza uzalendo fanya kwa manufaa ya Watanzania, hakikisha watu wanapata maji,”  amesema.

Akiwa katika kitongoji cha Kiembe kata ya Mapinga, Profesa Mbarawa amewaomba wakazi wa eneo hilo kutunza na kulinda miundombinu ya maji.

“Tumewaletea maji hakikisheni mnalinda miundombinu ili yaendelee kuwepo na vilevile mlipie ili watu wengine nao wafikishiwe huduma hii,” amesema.