VIDEO: Mamlaka ya Anga Tanzania yazuia ndege ya Fastjet kuruka, yaipa notisi ya siku 28

Muktasari:

  • Kutokana na mwenendo mbaya kibiashara wa Shirika la Ndege la Fastjet, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imetoa notisi ya siku 28 kufuta leseni ya shirika hilo pia imezuia kuruka kwa ndege yake kwa sababu za kiusalama.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania  (TCAA) imesema Shirika la Ndege la Fastjet limepoteza sifa ya kufanya biashara nchini, kuzuia ndege moja ya shirika hilo kuruka kutokana na matatizo ya mara kwa mara na kukosekana kwa meneja mwajibikaji wa shirika.

Hayo yamebainishwa na mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo, Hamza Johari leo Jumatatu Desemba 17, 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Amesema tayari TCAA imetoa notisi ya siku 28 kuanzia leo ya kusudio la kufuta leseni ya shirika hilo.

"Tumekuwa tukiwaandikia barua ya kuwataka watueleze kuhusu mwenendo wao wa biashara tangu Fastjet Plc wajiondoe lakini pia shirika limekuwa na madeni mbalimbali ambayo hayajalipwa. Tukiomba watupe mpango wao wa fedha na biashara kwa mujibu wa sheria hawafanyi hivyo," amesema Johari.

Amesema shirika hilo linadaiwa na watoa huduma wake wengi ikiwemo TCAA inayolidai Sh1.4 bilioni lakini pia halina meneja mwajibikaji ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ndege anayepaswa kutoa majibu ya hali ya ndege.

"Kwa sasa fastjet hawana ndege. Ndege yao tangu jana tumeizuia kuruka kwa kuwa imekuwa ikipata hitilafu mara kwa mara na hawana mtu ambaye anaweza kutoa taarifa kuhusu mwenendo wake jambo ambalo linahatarisha usalama endapo itaruka," amesema Johari.