Marie stopes wapigwa marufuku kutoa mimba

Muktasari:

  • Dk Marie Stopes alizaliwa mwaka 1880, Edinburgh nchini Scotland na kliniki yake ilitam-bulishwa kwa mara ya kwanza katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania mwaka 1989

Nairobi, Kenya. Bodi ya Wataalamu wa Madaktari Kenya (KMPDB) imelitaka Shirika la Marie Stopes kuacha kujihusisha na utoaji wa huduma za utoaji mimba kwa wanawake.

Bodi hiyo pia imeamuru, Shirika hilo kuondoa mara moja matangazo yanayoonyesha utoaji wa mimba ambazo hazitarajiwi zinazotangazwa kwenye tovuti zake kwa sababu ni kinyume cha sheria.

Bodi hiyo ilisema kwamba hospitali hizo zimekuwa zikitoa kwa siri kupitia kwenye tovuti kuwasaidia kwa siri wanawake kutoa ujauzito ambao haukutarajiwa jambo ambalo limedaiwa kuwa kinyume cha sheria pia.

Bodi hiyo imeuandikia uongozi na kuuambia kwamba sasa utoaji wa huduma hiyo ni kinyume cha sheria na kinaipotosha jamii kwa ujumla na pia bodi imekuwa ikipata malalamiko kutoka kwa jamii.

Agizo

Bodi imeamuru kituo hicho cha huduma kiache mara moja utaratibu wake wa utoaji mimba kwa wanawake wanaoizunguka jamii ya Kenya.

Pia, kuhusu matangazo wametakiwa kufuata sheria za matangazo ya huduma za tiba kama inavyotakiwa.

Daktari wa magonjwa ya wanawake wa Hospitali ya Kenyatta nchini Kenya, John Ongech alisema kwamba wanawake wengi nchini humo hawana uelewa wa utolewaji holela wa mimba.

“Ni vyema kuzaa mtoto wako kuliko kuchukua uamuzi wa kumtoa kwani unaweza ukapata madhara makubwa kwenye kizazi na huenda usipate tena mtoto utakapokuwa unamhitaji’’alisema

Zaidi ya wanawake 2,600 wanapoteza maisha kutokana na utolewaji wa mimba kiholela nchini Kenya ukilinganisha na nchi za Afrika Mashariki kwa mujibu wa kitengo cha Utafiti Wizara ya Afya Kenya.

Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa shirika hilo nchini Tanzania Dotto Mnyadi alipoulizwa kuhusu taarifa za hospitali hiyo kujihusisha na utoaji wa mimba, alisema hazina ukweli na kufafanua kuwa hawajawahi kuhusika na vitendo hivyo.

“Hospitali inatoa huduma ya mimba baada ya kuharibika (CPAC) hii ipo kisheria na kwa mwongozo wa Wizara ya Afya, japokuwa tunapokea idadi kubwa ya waliotoa mimba vichochoroni wanapofika hapa tunawahudumia ili kuokoa maisha,” alisema Mnyadi.

Tanzania

Dk Christopher Peterson anasema kwamba, utoaji wa mimba zisizopangwa na uzaaji holela usiofuata utaratibu wa uzazi mpango umepungua kwa kiasi kikubwa sana kutokana na matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

Alisema suala la matumizi ya njia za uzazi wa mpango linaweza kuibua maswali kadha wa kadha na kuleta mdahalo kwenye jamii zetu, na maswali haya wakati mwingine huwa tunakutana nayo sisi wahudumu wa afya; na baadhi ya maswali yanayoleta mjadala ni kama vile;

Je matumizi ya njia hizi mbalimbali za uzazi wa mpango zinazingatia usawa wa kijinsia?, Njia hizi za uzazi wa mpango ni rafiki kwa afya ya mtumiaji? (hasa mwanamke kama ilivyozoeleka).

Suala la kujikinga au kuzuia magonjwa ya zinaa imezoeleka kuwa ni jukumu la wote wawili yaani mwanaume na mwanamke wake, lakini suala la kuzuia mimba na kupanga uzazi wengi wanadhani kuwa ni jukumu la mwanamke. Na ndio maana inapofikia kwenye suala la kupanga uzazi mzigo wote wa kutumia njia mbalimbali za kupanga uzazi unabaki kwa mwanamke.

Alisema njia rahisi na ya asili ambayo mwanamke anaweza kuitumia katika kupanga uzazi, lakini haijaonekana kutumiwa na wanawake wengi kutokana na wanawake wengi kusema kuwa ni ngumu sana kuichunga ni kalenda na

hivyo kuwasababishia kujisahau, hivyo wanawake wengi hutumia njia mbadala kama vile vidonge, vitanzi, sindano na vinginevyo.

Kisayansi, pamoja na utendaji kazi wa njia hizi, lakini bado zimeonekana kuleta madhara mengine ya kiafya na madhara haya yanaweza kuwa ya muda mfupi au ya kudumu. Kuvurugika kwa mfumo wa homoni na mzunguko wa hedhi, hedhi iliyopitiliza au kukosa kabisa hedhi, maumivu ya tumbo, kiuno na mgongo wakati wa hedhi, na kupata uzito wa mwili uliopitiliza ni baadhi tu ya matatizo ya kiafya ambayo wanawake wengi huyapata kutokana na matumizi ya njia mbalimbali za uzazi wa mpango hasa kwa muda mrefu.

Matumizi ya njia za uzazi wa mpango si jukumu la mwanamke pekee hapana, ni jambo linalobeba usawa wa kijinsia.

Hata wanaume nao wana njia za uzazi wa mpango wanazoweza kuzitumia na kuwapunguzia wanawake majukumu haya na ikiwezekana kuwaondolea wanawake wao adha ya kupata matatizo ya kiafya yatokanayo na matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

Baadhi ya njia za uzazi wa mpango ambazo mwanaume anaweza kuzitumia ambazo ni rafiki kwa jinsia ya kiume ni pamoja na matumizi ya kondomu, njia ya kutoa mbegu za kiume nje wakati mwanamke akiwa kwenye siku za kushika mimba au ile inayohusisha upasuaji mdogo kwa lengo la kufunga mirija inayosafirisha mbegu za kiume kutoka kwenye korodani ili zisisafiri kwenda ukeni wakati wa tendo la ndoa.

Njia hii kitaalamu inaitwa vasectomy.