UCHOKOZI WA EDO: Mchakamchaka wa Anko Magu unatuacha hoi bin taabani

Muktasari:

Majuzi akina Charles wawili amewapiga benchi katika baraza lake. Ndani ya miezi 36 iliyopita kapiga chali mawaziri wake tisa bila ya kutangaza mabadiliko makubwa ya baraza la mawaziri. 

ANKO Magu pale Magogoni ananikumbusha kocha wa zamani wa Simba, Zdravko Logarusic. Hataki maisha ya kukariri. Yule kocha kutoka Croatia alikuwa anakupiga benchi muda wowote ule hata kama ametoka kukuingiza uwanjani dakika sita zilizopita. Ndivyo ilivyo kwa sasa. Anko ameondoa maisha yetu yote ya kukariri. Muda wowote anakuita benchi, anaingiza mchezaji mwingine, mechi inaendelea.

Majuzi akina Charles wawili amewapiga benchi katika baraza lake. Ndani ya miezi 36 iliyopita kapiga chali mawaziri wake tisa bila ya kutangaza mabadiliko makubwa ya baraza la mawaziri. Wamebaki 11 tu alioanza nao. Nilichogundua ni kwamba Anko ametuondolea habari nyingi ambazo zilikuwa kubwa katika vyombo vya habari. Sasa hivi zinakuwa habari za kawaida tu, zamani tulikuwa tunauza magazeti yetu kwa habari za kuondolewa kwa mawaziri. Siku hizi hatuuzi sana.

Zamani Escrow au EPA zilipoondoka na vichwa vya watu ilikuwa habari kubwa. Asubuhi ukipita vituo vya daladala na kuchungulia meza za magazeti unakuta watu wamejaa. Wananunua magazeti na kusoma ‘Mzee wa Vijisenti Out’. Siku hizi sio habari kubwa.

Anko anafanya sub kila siku na bahati nzuri karibu kila mtu anajua kujumlisha hesabu zake. Unajua tu kwamba Charles huyu kaondoka kwa sababu hii, na Charles mwenzake akaondoka kwa sababu fulani. Mchezo umekwisha.

Wakati mwingine Anko anaweza kuharibu biashara kabisa kwa sababu wakati unapojaribu kuchunguza sababu ya kwa nini fulani ameondolewa ili uuze habari, yeye ndio kwanza anafichua siri mbele za watu. Wala hafichi. Anatuua njaa wauza habari. Mchakamchaka wa maisha ya Anko kwetu ni mzito. Tupo taabani. Anatufundisha tuache kuishi kwa kukariri lakini hata kwa wanaopigwa benchi wanafundishwa kujua kuishi vema na jamii katika zama hizi.

Kwa mfano, kwa sasa mawaziri lazima wawe na namba za simu za madereva teksi. Muda wowote unaweza kutumbuliwa ukiwa ‘Transiti’ Nairobi unarudi Dar. Unashangaa dereva hajafika kukupokea. Kumbe Dereva aligeuza gari wakati ndege iliyokubeba ikiwa usawa wa Mlima Kilimanjaro. Unatua Airport, unapokea habari ya kutumbuliwa, unampigia dereva teksi unaondoka. Tuendelee kujipanga sana katika maisha ya Anko, tusikariri.