Mufti aeleza mipango ya kisasa ya Bakwata

Muktasari:

Kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata) yatakayofanyika jijini Dar es Salaam Desemba 17, 2018, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi ameeleza mipango itakayolifanya baraza hilo kuwa la kisasa


Dar es Salaam. Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi ameeleza mipango itakayolifanya Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata)  kuwa la kisasa zaidi.

Zuberi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi 13, 2018 wakati akifungua semina  ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya Bakwata itakayofanyika jijini hapa Desemba 17, 2018

“Tukimuona kiongozi haileweki wala halitetei baraza hili, nyie mnadhani tumfanyeje ebu semeni nyie. Hivi mtu huyo anatufaa au hatufai” Sheikh Zuberi aliwahoji masheikh waliohudhuria ambao walijibu “hatufai.”

Sheikh Zuberi amesema kiongozi wa aina hiyo hawafai na atawarudisha nyuma katika jitihada zao lakini wataendelea kuwasiliana naye kupitia masuala  mbalimbali na  kubadilisha mawazo.

“Huku kwenye kuongoza baraza yeye hatufai. Ujamaa na urafiki utaendelea kama kawaida lakini kwenye uongozi hapana,” amesema.

Kuhusu maslahi ya Waislamu,  kiongozi huyo amesema waumini wa dini wanahitaji kuona Bakwata inawatendea masuala yenye uhitaji kwao. Miongoni mwa masuala hayo ni kutazamwa, kuwa karibu nao, kushughulikia matatizo yao.

“ Haya ndio maslahi yao lazima tuyaangalie  sisi viongozi kwa nafasi zetu tulipo. Tuelewa tuna dhima kubwa kwa waumini hawa,” amesema Sheikh Zuberi.

Akifafanua kuhusu maslahi ya Taifa, Sheikh Zuberi amesema hawezi kuwa ndani ya Bakwata halafu ukalisaliti Taifa kwa kuwa ni mlinzi wa nchi na ana watu nyuma.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum amesema semina hiyo imejumuisha masheikh wa wilaya na kata zote za mkoa huo kwa lengo la kuwajengea uwezo kabla ya kuadhimisha miaka 50 ya Bakwata.