Mwenyekiti wa mtaa alia kukithiri kwa mauaji mtaani kwake

Mwenyekiti wa Mtaa wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, Bakari Shingo

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa mtaa wa Gongo la Mboto amezungumzia kukithiri kwa mauaji katika mtaa huo, akibainisha kuwa tangu 2016 hadi leo Jumatatu Desemba 10, 2018 wameuawa watu 11

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Mtaa wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, Bakari Shingo amelalamikia matukio ya mauaji katika mtaa huo, akidai kuwa tangu Desemba 2016 hadi leo Jumatatu Desemba 10, 2018 watu 11 wameuawa.

Shingo amesema imebainika kuwepo kwa kikundi kinachoratibu mauaji hayo ambayo amedai hutokea zaidi ikifika mwezi Novemba, Desemba na Januari.

Amesema tukio jingine limetokea Desemba 7, 2018  baada ya  kijana mmoja kukutwa amechinjwa na mwili wake kutupwa pembeni ya reli.

Shingo ambaye pia ni mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Ilala  wilaya ya Ilala amesema kuwa mara kadhaa amefanya mawasiliano na Jeshi la polisi lakini hakuna hatua zilizochuliwa.

Wahusika wanafahamika lakini hadi leo hakuna aliyekamatwa, nimechoshwa na mauaji haya kwenye mtaa wangu naomba mnisaidie kupaza sauti,” ameeleza Shingo.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi Ilala, Ernest Matiku amesema kilichozungumzwa hakina ukweli.

Amesema  hakuna ushahidi unaoachwa na polisi na watuhumiwa wote wanahojiwa  kama taratibu zinavyoelekeza