Dk Slaa: Ninalindwa na Usalama wa Taifa

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema Dk.Wilbroad Slaa.

Muktasari:

Dk Slaa alitangaza kujiondoa kwenye siasa za vyama Septemba mosi, akieleza kuwa alitofautiana na viongozi wenzake wa Chadema kuhusu namna ya kumpokea Edward Lowassa kutoka CCM ili awe mwanachama na mgombea urais, na akatumia fursa hiyo kumrushia ‘makombora’ mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya Ukawa.

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod Slaa juzi alijitokeza tena hadharani kujibu mapigo ya hoja mbalimbali zilizojitokeza wakati akitangaza kustaafu siasa za vyama, akiweka bayana kwamba hivi sasa analindwa na usalama na amehama nyumbani kwake.

Dk Slaa alitangaza kujiondoa kwenye siasa za vyama Septemba mosi, akieleza kuwa alitofautiana na viongozi wenzake wa Chadema kuhusu namna ya kumpokea Edward Lowassa kutoka CCM ili awe mwanachama na mgombea urais, na akatumia fursa hiyo kumrushia ‘makombora’ mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya Ukawa.

Hotuba yake ilizua maswali mengi, ikiwa ni pamoja na gharama alizotumia kurusha moja kwa moja mkutano na wake na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Serena, huku mkewe wa zamani akijitokeza kukanusha kuishi maisha ya shida, huku Ukawa ikisema alikuwa akiutaka urais, tofauti na maelezo yake.

Akihojiwa kwenye kipindi maalumu kilichorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Star Tv juzi usiku, Dk Slaa alisema sambamba na kuhamia Hoteli ya Serena, ambayo ni ya kiwango cha nyota tano, hata nyumba yake inalindwa na usalama wa taifa.

“Nakaa Serena kwa sababu ninapata vitisho, nilishasema kuwa kipindi hiki nimepata vitisho vingi kuliko nilivyopata wakati nilipotaja orodha ya mafisadi. Watanzania hawajui jinsi mimi na familia yangu tunavyoishi,” alisema.

Katika mazungumzo yake na Star Tv yaliyodumu kwa dakika 85, Dk Slaa alisema amekuwa akipata vitisho vingi, vinavyoiweka familia yake hatarini huku akieleza jinsi mke wake, Josephine Mushumbusi alivyokoswakoswa na risasi akiwa kwenye gari.

“Si ajabu mimi kulindwa na Usalama wa Taifa. Ingawa nilishawahi kuwasema hawa watu wa usalama, sasa wananilinda na ni utaratibu kuwa ukiomba ulinzi kwa utaratibu unaotakiwa, unapewa,” alisema.

Alifafanua zaidi kuwa ameshtushwa na uzushi ulionezwa kuwa amekimbilia Marekani, akisema hajawahi kufanya hivyo, bali aliwahi kwenda nchini humo mwaka jana katika kazi zake za siasa.

“Niliwahi kwenda Marekani mwaka jana katika kazi zangu za siasa na nikatembelea majimbo 13. Gharama hizo nilijilipia mwenyewe, nilikwenda kujifunza mambo fulani fulani ya uongozi,” alisema.

Soma zaidi haabri hii kupitia Mwananchi-Epaper