Nusu ya madai ya wazee wa mabaraza ya Mahakama si sahihi

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde akizungumza bungeni alipokuwa akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Madai yenye thamani ya Sh55.5 milioni kati ya Sh115.45 milioni wanayodai wazee wa mabaraza ya Mahakama kama malimbikizo ya posho zao yamebainika kuwa siyo halali- Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Antony Mavunde amesema hayo.

Dodoma.  Madai yenye thamani ya Sh55.5 milioni kati ya Sh115.45milioni wanayodai wazee wa mabaraza ya Mahakama kama malimbikizo ya posho zao yamebainika kuwa siyo halali.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Antony Mavunde alisema hayo bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Silafu Jumbe Maufi  kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria.

Silafu alisema ukomo wa bajeti tangu mwaka 2016/17 na 2018/19 hauko rafiki kwa Mahakama kukamilisha majukumu yake hasa kuwalipa wazee wa mabaraza ya Mahakama.

“Je Serikali inawaangalia vipi wazee hao kwa malimbikizo ya posho zao na je inachukua hatua gani kuhusu kuongeza posho za wazee wa mabaraza ya Mahakama?” alihoji Silafu.

Akijibu, Mavunde alisema Serikali inatambua mchango wa wazee wa mabaraza ya Mahakama katika kutoa haki kwa wananchi.

Alisema mwaka wa fedha 2017/18 Serikali ilifanya uhakiki wa malimbikizo ya posho za wazee wa mabaraza hayo yenye thamani ya Sh115.45 milioni na kubaini kuwa malimbikizo halali yalikuwa ni Sh59.96 milioni (sawa na asilimia 52) ya madai yote.

Alisema kiasi kilichosalia cha Sh55.5milioni kilibainika kuwa siyo halalli kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kukosekana kwa vielelezo au uthibitisho wa kumalizika kwa mashauri husika na fomu za uthibitisho wa madai.

“Hivyo Serikali imechukua hatua kwa kuanza kulipa malimbikizo yaliyohakikiwa na yanategemewa kukamilika Desemba 2018,” alisema.

Alisema viwango vya malipo wanavyolipwa wazee hao kwa sasa havilingani na hali halisi na muda unaotumika kutoa huduma hiyo.

Alisema kwa kuzingatia hilo Mahakama ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2018/19 imeanza kulipa nauli, posho ya chakula kwa wazee wote wa mabaraza wanaoitwa kushiriki katika mashauri ya vikao ngazi ya Mahakama Kuu.

Mavunde alisema Serikali itaendelea kuboresha viwango vya posho kwa kadri bajeti ya Mahakama itakavyoruhusu.