VIDEO: Profesa Assad, Ndugai wazua mjadala mtandaoni

Muktasari:

  • Unaweza kusema kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kumtaka CAG, Profesa Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kwa hiyari imezua mjadala mkali mtandaoni

Dar es Salaam. Unaweza kusema kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kwa hiari kwa ajili ya kuhojiwa, imezua mjadala mkali mtandaoni.

Ndugai ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 7, 2019 mjini Dodoma katika mkutano wake na waandishi wa habari akimtaka pia Profesa Assad ajitathmini kama anatosha katika nafasi yake.

Ndugai amesema Profesa Assad amelidhalilisha Bunge kutokana na kauli yake kuhusu chombo hicho cha dola aliyoitoa katika mahojiano na

Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Katika mahojiano hayo mtangazaji, Arnold Kayanda alimhoji kuhusu ukaguzi unaofanywa na ofisi yake kuonekana na wananchi kuwa haufanyiwi kazi, msomi huyo kusema huo ni udhaifu wa Bunge.

 

“Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa,” alisema Profesa Assad.

 

Aliongeza: “Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.”

Kwa nyakati tofauti kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter wamefunguka na kuelezea mazito juu ya kauli hiyo ya Spika Ndugai huku baadhi wakipinga kuwa hana mamlaka hayo.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amesema wito alioutoa Ndugai ni dharau kubwa kwa taasisi za uwajibikaji na ni dalili za kulewa madaraka.

“Watanzania tusikubali CAG (mlinzi wa fedha zetu) kudhalilishwa. Tunajua hizi ni mbinu za kumkatisha tamaa Profesa Assad katika utendaji wake. Tusikubali CAG adhalilishwe kwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Bunge,” amesema Zitto.

“Hilo likitokea ni sawa na kuua kabisa uhuru wa CAG. Kila mtu afikirie njia bora na sahihi ya kumzuia Spika Ndugai kufanya dhambi hii mbaya kabisa.”.

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema katika ukurasa wake wa Twitter amesema kulingana na mambo yanavyoendelea nchini kuhusu matamko kuna siku mkuu wa wilaya anaweza kutoa amri ya kiongozi wa ngazi ya juu kuwekwa kizuizini na ikatekelezwa.

“Kuna wenge la hatari sana. Mpaka hujui nani mkubwa na nani mdogo, ukiharibu utawala bora hakuna kingine. Sio msingi tena katika nchi ni dhahiri kabisa kuwa CAG Assad pamoja na kulindwa na Katiba na sheria bado anaweza akavaa pingu kama Spika alivyosema,” amesema Lema.

Mwananchi mwingine Martin M. M ameandika, “Spika wa Bunge asiyefahamu hata Sheria za nchi ambazo Bunge limezitunga hajui kabisa kwamba katiba ya Tanzania 143(6) sambamba na Sheria ya ukaguzi wa umma 3.14, hakuna mamlaka yenye uwezo wa kumhoji CAG isipokuwa tu kwa mashtaka mahakamani.”

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume ameandika, “Nimeshaelewa Spika anatumia s. 24 ya Parliamentary Privileges and Immunities Powers Act eti CAG ka commit contempt. Hiyo section inatumika pale mtu kaitwa kama shahidi bungeni na akakosa nidhamu sio pale mtu anaikosoa Bunge akiwa nje ya Bunge.”

Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ameandika, “Kama kunakosa lilifanyika basi ni kumteua Profesa Assad kuwa CAG. Mtu mwenye hofu ya Mungu kama yule hajui kusema uongo, haendeshwi na mahitaji ya tumbo,  atawasumbueni.”