Sekta binafsi yataka utekelezaji maagizo ya JPM

Mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa la Wakurugenzi wa Sekta Binafsi (CEOrt), Ali Mufuruki

Dar es Salaam. Wadau wa sekta binafsi wamekuwa na maoni tofauti baada ya hotuba ya Rais John Magufuli aliyezitaka mamlaka za usimamizi nchini kufanya kazi kwa weledi ili kuhamasisha uwekezaji.

Wakizungumza na Mwananchi jana, wadau hao akiwamo katibu mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye walikuwa na maoni tofauti.

Simbeye alisema licha ya kupunguza wingi na viwango vya kodi kama Rais alivyoagiza, ipo haja ya kurekebisha utungaji wa sera za fedha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) isiwe mtungaji na msimamizi kwa wakati mmoja.

“Tunahitaji muda wa kutosha kujadili mabadiliko ya kodi. TRA inatakiwa kutekeleza kitakachojadiliwa na wadau,” alisema.

Mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa la Wakurugenzi wa Sekta Binafsi (CEOrt), Ali Mufuruki alisema tatizo kubwa lililopo nchini ni udhaifu wa sekta binafsi.

“Tumekuwa tukizungumza kuhusu mazingira magumu ya uwekezaji na haja ya kuboresha mfumo wa kodi nchini, lakini hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa. Hali hiyo, imesababisha biashara nyingi kufungwa,” alisema Mufuruki.

Makamu wa rais wa Chama cha Wasafirishaji (TAT), Omar Kiponza alisema hoja ya askari kuwapotezea muda wafanyabiashara wanaoenda nje ya nchi imetolewa wakati muafaka.

“Kasi ya ukamataji ni kubwa na mafaili ya kesi husika yanarundikwa kwenye vituo vya polisi hivyo kuchelewesha usafirishaji wa mizigo,” alisema.

Hata hivyo, Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kilitoa pongezi kwa msimamo wa Rais. Katibu mkuu wa chama hicho, Enea Mrutu alisema kusimamishwa hovyo ni kero ya muda kwao hali inayopunguza ufanisi.

“Namshukuru Rais Magufuli kwa kuliona hili. Haya mambo yametukera kwa muda mrefu wasafirishaji. Kitendo cha kusimamishwa ovyo kinasababisha magari kutomaliza safari hivyo kulala njiani. IGP Sirro (Mkuu wa Jeshi la Polisi-Simon), ajipange na askari wake,” alisema Mrutu.

Mjumbe wa bodi ya Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Rahim Dosa alisema Rais ametoa msimamo sahihi utakaosaidia kuwapunguzia kero.

“Unaposimamishwa kwa muda mrefu ndivyo unavyochelewa na kusababisha gharama za uendeshaji kuongezeka. Yaani hapa siongezi kitu maana Rais Magufuli kamaliza, hili jambo linatuumiza sana,” alisema Dosa.

Licha ya onyo hilo kwa trafiki, Dosa anakumbuka jinsi Rais Magufuli alivyoagiza kupunguzwa kwa idadi ya mizani kutoka saba hadi mitatu kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma mkoani Songwe.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Silver Siondo alisema kupunguza viwango vya kodi kutasaidia kuongeza uwazi na ulipaji wa hiari kwakuwa wengi wanaviogopa viwango vikubwa vilivyopo.

Kutokana na hali hiyo, alisema wanapoagiza mizigo kutoka nje hawaweki wazi gharama halisi kuhofia kodi kubwa.

“Ukiwepo unafuu kwenye makadirio, ikawekwa kodi inayolipika, watu watalipa kwa hiyari na TRA watakusanya zaidi,” alisema.

Alitahadharisha kwamba endapo hakutakuwa na umakini, vitambulisho hivyo vinaweza kuchukuliwa na wajanja watakaotaka kujificha miongoni mwa wamachinga hivyo kuikosesha Serikali mapato stahiki.

Akitoa maoni yake, mkurugenzi wa sera wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Akida Mnyenyelwa alisema kuna suala la gharama kubwa za uzalishaji ambalo lina athiri ushindani wao kwenye soko la kimataifa.

“Viwanda vilivyosajiliwa nchini ni vichache ambavyo vinatozwa kodi kila siku lakini walipa kodi wakiwa wengi itapunguza kiwango na kuongeza mapato ya Serikali,” alisema.

Imeandikwa na Cledo Michael, Bakari Kiango na Ludger Kasumuni

Makamu wa rais wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Octavian Mshiu alisema alipongeza agizo la kuzitaka mamlaka za udhibiti kufanyakazi kwa pamoja ili kupunguza urasimu.

“Kuna muingiliano wa majukumu miongoni mwa mamlaka hizi, tunapendekeza wachanganywe na iwe leseni moja ili kuondoa mlolongo mrefu uliopo unaotupunguzia ushindani wa kibiashara,” alisema.

Imeandikwa na Cledo Michael, Bakari Kiango na Ludger Kasumuni